Na Mwandishi Wetu
Serikali imetoa ufafanuzi rasmi kufuatia kusambaa kwa taarifa za upotoshaji kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa kiasi cha shilingi bilioni 730 ni bajeti mpya iliyotengwa maalumu na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na mvua za El Niño.
Serikali imefafanua kuwa kiasi hicho si fedha mpya iliyotengwa pekee, bali ni jumla ya makadirio ya rasilimali na bajeti zilizowasilishwa na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali kupitia Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Ufafanuzi huoi umetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mnafanikio ya utekelezaji wa mkiradi ya maendeleo ya wananchi, Jijini Dodoma leo.
"Ndugu Waandishi wa Habari; Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika kulinda maisha, usalama na mali za wananchi kwa kuchukua hatua za tahadhari na kuandaa mazingira wezeshi ya kuzuia na kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na majanga mbalimbali.
Alisema mpango huo ulioratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu unajumuisha shughuli za kukarabati miundombinu ya barabara, madaraja na mitaro, ununuzi wa chakula cha akiba, vifaa vya uokoaji, pamoja na maandalizi ya makazi ya muda katika maeneo hatarishi ili kulinda maisha na mali za wananchi kutokana na utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania unaoonyesha uwezekano wa kuwepo kwa mvua hizo zenye nguvu kubwa.
Alisema katika kuendeleza juhudi hizo, Serikali imeandaa Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kwa kuzingatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na umuhimu wa kuchukua hatua za mapema ili kulinda maisha na mali za wananchi na kwamba video inayosambaa katika mitandao ya kijamii yenye taarifa zinazopotosha kuhusu makadirio ya bajeti ya shilingi bilioni 730 yaliyoainishwa katika mpango huo, sio sahihi imejaa upotoshaji.
Akifafanuzi zaidi alisema maandalizi yanayoendelea kufanywa na Serikali kukabiliana na madhara yanayoweza kusababishwa na El Niño, ni mkusanyiko wa shughuli zilizopangwa kutekelezwa na makadirio ya bajeti kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa, mashirika ya kitaifa na kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, pamoja na taasisi zisizo za kiserikali.
Alisema taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri unaoonesha uwezekano wa kutokea kwa hali ya El Niño yenye nguvu (Strong El Niño), inayoweza kusababisha mvua kubwa na kuleta madhara mbalimbali, yakiwemo mafuriko, maporomoko ya ardhi, magonjwa ya mlipuko kwa binadamu na wanyama, pamoja na majanga mengine yanayohusiana na mvua hizo na hivyo serikali lazima ijiandae.
Alisema kufuatia utabiri huo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) iliratibu maandalizi ya Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño ambapo makadirio ya bajeti na shughuli zilizopangwa na taasisi hizo yaliwasilishwa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambapo kwa kushirikiana na wataalamu kutoka sekta husika, uliandaliwa mpango jumuishi wa kitaifa wa kujiandaa na kukabiliana na madhara ya El Niño.
"Serikali inapenda kusisitiza kuwa makadirio ya rasilimali ya shilingi bilioni 730 yaliyoainishwa katika mpango huo yanajumuisha bajeti za taasisi za Serikali na zisizo za Serikali . Hivyo, kiasi hicho si bajeti mpya inayotengwa na Serikali kwa ajili ya kukabiliana na El Niño pekee, bali ni jumla ya makadirio ya rasilimali zinazohitajika kutekeleza shughuli mbalimbali zilizoainishwa katika mpango huo" alisema Msigwa.
Alisema kuwa taasisi husika zitatekeleza majukumu yao kwa kutumia rasilimali zilizopo ndani ya taasisi hizo, kwa kuzingatia bajeti zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027. Alisema katika utekelezaji huo, kipaumbele kitatolewa kwa shughuli zinazolenga kuwahudumia wananchi watakaokumbwa na madhara ya mvua za El Niño.
Aidha, alisema makadirio ya bajeti yaliyowasilishwa na taasisi za Serikali na zisizo za Serikali yamezingatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na uchambuzi wa madhara yanayoweza kujitokeza katika sekta mbalimbali kutokana na hali ya El Niño katika mwaka wa fedha 2026/2027. Kwa mujibu wa utabiri huo wa TMA, hali hiyo inatarajiwa kuwa na nguvu kubwa kuliko zilizotokea katika miaka ya 2023/2024, 2015/2016 na 1997/1998.
Alisema Mpango wa Taifa wa Dharura wa Kujiandaa na Kukabiliana na Madhara ya El Niño umeandaliwa kwa lengo la kuimarisha utayari, kuongeza uwezo wa kukabiliana na majanga, na kuwezesha kuchukuliwa kwa hatua za mapema na za pamoja katika kuzuia, kujiandaa, kukabiliana na kurejesha hali baada ya kutokea kwa madhara ya El Niño.
Mpango huo umezingatia Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Maafa ya mwaka 2004, Toleo la mwaka 2025, pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Sura ya 242. Utekelezaji wa mpango huo utahusisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa, mashirika ya kitaifa na kimataifa, mashirika ya Umoja wa Mataifa, asasi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, sekta binafsi, mashirika ya kijamii na vyombo vya habari. Kwa sasa, taasisi hizo zinaendelea kutekeleza baadhi ya shughuli zilizoainishwa katika mpango huo kwa kutumia bajeti za kisekta zilizoidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Shughuli zilizopangwa katika mpango huo zimejikita katika kukarabati na kuboresha miundombinu ya barabara, madaraja na mitaro, pamoja na miundombinu ya huduma za kijamii katika maeneo hatarishi. Huduma hizo ni pamoja na afya, elimu, usafiri, nishati ya umeme, maji safi, maji taka na mawasiliano.
Shughuli nyingine ni ununuzi na uhifadhi wa akiba ya taifa ya chakula, hususan nafaka; ununuzi wa vifaa vya uokoaji; uwekaji wa misaada ya kibinadamu katika maghala ya kikanda; maandalizi ya makazi ya muda kwa ajili ya kuwahifadhi wananchi watakaolazimika kuhama maeneo yao endapo maafa yatatokea; pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu hatua za kuzuia na kupunguza madhara, kujiandaa na kukabiliana na maafa, na kurejesha hali baada ya majanga kutokea. Majanga yanayolengwa katika shughuli hizo ni pamoja na mafuriko, radi, maporomoko ya ardhi na magonjwa ya mlipuko.


0 Comments