Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, amesema Mkoa wa Pwani unatarajia kufungua rasmi Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote tarehe 22 Oktoba 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya bila kukabiliwa na mzigo mkubwa wa gharama za matibabu.
Mhe. Nyongo ameyasema hayo leo, Oktoba 20, 2026, na kubainisha kuwa ufunguzi huo utafanyika katika viwanja vya standi ya zamani Maili Moja alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha, ambapo amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Pwani kujitokeza kujiunga na mpango huo unaotekelezwa kwa mujibu wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023.
Amesema mpango huo unalenga kulinda afya na uchumi wa wananchi kwa kuhakikisha kuwa wanapokabiliwa na changamoto za kiafya, wao na familia zao hawalazimiki kuuza mali au kukopa fedha ili kugharamia matibabu.
“Afya ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii. Mwananchi anapokuwa na afya njema anaweza kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, biashara, uvuvi na shughuli nyingine za kiuchumi. Bima ya afya ni kinga inayosaidia kulinda afya na ustawi wa familia,” amesema Mhe. Nyongo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya bila kujali kipato chao au eneo wanaloishi.
Akizungumzia kaulimbiu ya uzinduzi huo,ambayo ni “Bimika na Fahari ya Bima,” Mhe. Nyongo amesema inalenga kuhamasisha wananchi kutambua umuhimu wa kujiunga na bima ya afya kama hatua ya kujilinda dhidi ya gharama za matibabu na kupanga maisha ya familia zao.
Akitoa takwimu za utekelezaji wa awamu ya kwanza Mhe. Nyongo amesema hadi Oktoba 20, 2026, jumla ya kaya 4,463, sawa na asilimia 72 ya kaya lengwa 6,212, zilikuwa zimesajiliwa katika mpango huo.
Katika Awamu ya Pili, Mkoa wa Pwani umelenga kusajili kaya 12,872 zenye jumla ya wanufaika 23,304. Katika maandalizi ya awali, kaya 1,640 zenye wanufaika 2,296 zimefanyiwa uhakiki na kusajiliwa.
Mhe. Nyongo amewahimiza wananchi kutumia fursa hiyo kujiunga na mpango huo kwa kuchangia shilingi 150,000 kwa kila kaya yenye watu sita, akisisitiza umuhimu wa kujiandaa mapema kwa kuwa ugonjwa unaweza kumpata mtu wakati wowote.
Vilevile, amevitaka vyombo vya habari kuwa mabalozi wa kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kutumia redio, magazeti, televisheni na majukwaa ya kidijitali ili kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wananchi wengi zaidi.
Uzinduzi rasmi wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote Mkoa wa Pwani unatarajiwa kufanyika Oktoba 22, 2026, katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Maili Moja, Kibaha, ambapo wananchi pia watapata huduma mbalimbali za upimaji wa afya bila malipo.

0 Comments