RC NYONGO: “SIKO PWANI KUKAA OFISINI, NIMEKUJA KUWASIKILIZA WANANCHI”

 

Mkuu wa Mkoa wa Pwani Stanslaus Nyongo. 


Msata Pwani:

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Stanslaus Nyongo, amesema ameteuliwa kuongoza Mkoa wa Pwani kwa lengo la kuwasikiliza wananchi, kushughulikia kero zao na kushirikiana nao kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

Mhe. Nyongo ameyasema hayo Oktoba 7, 2026, wakati wa ziara yake katika Kata ya Msata, Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze, alipokutana na wananchi katika mkutano wa hadhara wa kusikiliza na kutatua kero zao.

Akizungumza katika mkutano huo, RC Nyongo amewatoa hofu wananchi kwa kusisitiza kuwa uwepo wake mkoani humo si kwa ajili ya kukaa ofisini pekee, bali ni kuhakikisha anawafikia wananchi, anawasikiliza na kufuatilia changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi.

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Mkoa amewaomba wananchi walioondoka katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za Jeshi kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa za kweli wakati wa zoezi la uthamini linalotarajiwa kurudiwa.


Amesisitiza kuwa ukweli na ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kuhakikisha mchakato wa uthamini unafanyika kwa utaratibu unaofaa na kuwezesha malipo stahiki kufanyika kwa mujibu wa taratibu na sheria.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuwasikiliza wananchi moja kwa moja, kupokea kero zao na kufuatilia hatua za kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili katika Mkoa wa Pwani. 

Post a Comment

0 Comments