ZEGE HAILALI KAZI ZIMALIZIKE KWA WAKATI NA VIWANGO -DKT KIJAJI

 

Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ameeleza kuwa jitihada za

Ngorongoro kuboresha miundombinu ya Utalii eneo la maporomoko ya maji na

mapango ya Tembo Endoro ni silaha muhimu kutekeleza ilani ya CCM ya kufikisha

Watalii milioni nane mwaka 2030 na kuitaka menejimenti kuendelea kusimamia ujenzi huo kwa kasi na viwango.

Akielezea  kufurahishwa kwake kutokana na kasi ya ujenzi katika eneo hilo, waziri Dkt. Kijaji amesema fedha za utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na mfuko wa maendeleo ya utalii (TDL) zipo na hivyo ni jukumu la Mamlaka kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.

Ameeleza kuwa  hadi sasa Ngorongoro imetengewa shilingi bilioni 10 kwa utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo barabara ambapo wakandarasi wameendelea kulipwa kwa kila hatua na fedha ipo.

Mhe. Kijaji amebainisha  kuwa kati ya fedha hizo shilingi 1,674,783,089.00  zitatumika kwa ajili ya miradi ya kivutio cha utalii Endoro na Ngoitoktok vilivyopo eneo la hifadhi ya Ngorongoro ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 68 na mradi utakamilika mwezi Desemba, 2026.

Msimamizi wa Mradi huo SACC Mariam Kobelo ameeleza kuwa mradi wa Endoro unahusisha majengo ya Ofisi, geti, walking trails zenye urefu wa mita 2,200, boardwalk, alama za maelekezo, vyoo na maeneo ya kupumzikia wageni wakati katika eneo la Ngoitoktok mradi unalenga kuboresha mazingira eneo la picnic kwa kuongeza miundombinu ya kukaa na kupumzika kwa wageni.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa barabara ya tabaka gumu kutoka Loduare hadi geti la Seneto km 29.5 Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro Abdul-Razaq Badru ameeleza kuwa mradi huo unaotekelezwa kwa miaka miwili kwa thamani ya shilingi Bilioni 80.36 unaendelea vizuri ambapo hadi sasa umefikia asimilia 8 ambapo nguvu kazi na usimamizi unaendelea kuimarisha ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.


Post a Comment

0 Comments