Dar es Salaam, tarehe 7 Novemba, 2026.
Waswahili husema *Hayawi hayawi sasa yamekuwa na Mwanzo wa Ngoma ni Lele,* na sasa Ngoma inachezwa kufuatia *Ngorongoro Scholarship Fund* iliyozinduliwa tarehe 4 Agosti, 2026 kuwezesha wanafunzi waishio hifadhi ya Ngorongoro kupata fursa ya elimu ambapo *wanafunzi 14 wamepatikana na kuagwa leo* Jijini Dar es Salaam kuelekea Vyuo vikuu mbalimbali.
Kamishna wa Uhifadhi Ngorongoro *Dkt. Abdul-Razaq Badru* ameeleza kuwa kupitia *Ngorongoro Scholarship Fund* , *NCAA* kwa kushirikiana na *Bodi ya Mikopo* baada ya uchambuzi jumla ya *wanafunzi 14* wamekidhi vigezo na kuchaguliwa kujiunga Vyuo vikuu ambavyo ni *Chuo kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori-MWEKA, Chuo cha Uhasibu Arusha (AIA) na chuo Kikuu cha SAUT* ambapo wamedahiliwa katika masomo ya u *Uhifadhi wa Wanyamapori, misitu, Malikale na utalii.*
“ *Kupitia Ngorongoro Scholarship Fund tumetenga Milioni 100* mwaka huu kufadhili wanafunzi, tunaamini wanafunzi hawa wakimaliza masomo yao itawawezesha kujiajiri ama kuajiriwa maeneo mbalimbali Serikalini na Sekta binafsi, Utekelezaji wa program hii ni utekelezaji wa majukumu matatu ya Ngorongoro katika uhifadhi, utalii na kuwaendeleza wakazi waishio ndani ya Hifadhi. Ufadhili huu unalenga kusaidia wenyeji wenye sifa za kupata elimu ya vyuo vikuu, mpango huu utatekelezwa kila mwaka kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo kwa kuzingatia muongozo wa utoaji wa mikopo” amesema Dkt. Badru.
Mkurugenzi Mkuu wa *Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu Dkt. Bill Kiwia* ameeleza kuwa kupitia *Ngorongoro Scholarship Fund* Bodi hiyo ilipokea *maombi 26 na baada ya kuchakata jumla ya wanafunzi 14* walikidhi vigezo na kunufaika na ufadhili huo kwa kuzingatia misingi ya haki, usawa na uwazi kwa wote wanaostahili na kuongeza kuwa kwa wanafunzi 14 waliopatikana jumla ya shilingi Milioni 70.6 itatumika kufadhili gharama za masomo yao ili kutimiza ndoto zao za kupata ujuzi, fursa ya kusaidia taifa katika shughuli za uhifadhi, utalii, mazingira.
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Wafugaji *Ngorongoro Mhe. James Moringe* *ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kwa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 93 wa Sekondari, wanafunzi 33 wa kidato cha 5 na 6, wanafunzi 36 ngazi ya vyuo vya Kati na wanafunzi 14* waliopata ufadhili wa vyuo vikuu mwaka huu.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wanafunzi wenzake, *Ndina Koyaki Mollel kutoka kata ya Alailelai* ameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kufikia ndoto ya kupata elimu iwe fursa kwao kujiajiri, kuajiriwa na kusaidia familia zao na kuiomba serikali kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosajiliwa kwa miaka ijayo.

0 Comments