EMPAKAAI KRETA KIVUTIO KWA WATALII

Kasoko ya Empakaai ni mojawapo ya Kasoko za volkano ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, ikiwa na kingo za juu na ziwa zuri linalofunika zaidi ya asilimia 75 ya sakafu ya Kreta/Kasoko. Kivutio kikubwa ndani ya kreta hii ni idadi kubwa ya ndege heroe (flamingo) wanaoonekana kando ya ufukwe wa ziwa, Ndege wanapokuwa wengi hufanya ziwa hilo kuwa na rangi ya pinki.

Kreta hii katika nyanda za juu za Ngorongoro imezungukwa na kuta za misitu yenye mteremko mkali wa takribani mita 300 kwa urefu, zikiwa na uoto wa asili wa kijani kibichi, wanyamapori na aina mbalimbali ya ndege. Eneo lake lina upana wa takribani kilomita 8, huku karibu nusu ya sakafu yake ikifunikwa na ziwa la lenye magadi na kina kirefu, makazi ya heroe (flamingo) na ndege wengine wa majini.

Kutoka juu ya ukingo wa kreta ya Empakai, wageni wanaweza kuona Mlima Oldoinyo Lengai, Bonde la Ufa na Ziwa Natron kwa mandhari ya kuvutia. Pia wanaweza kufurahia matembezi ya asili kutoka juu ya mlima au kushuka hadi sakafuni kushuhudia vivutio vilivyopo.

Empakaai ina kimo cha takribani mita 3,200 kutoka juu ya usawa wa bahari upande wa magharibi na mita 2,590 upande wa mashariki. Mara nyingi hufunikwa na ukungu kutokana na mwinuko wake ambapo ziwa huonekana la kijani kibichi au buluu ya kina.

Kreta/Kasoko ya Empakaai ni maarufu kwa safari za kutembea kwa miguu, ambapo watalii hutembea kwa takribani saa mbili na nusu kwenda na kurudi kutegemea na uwezo wa mwili. Wageni wanaweza kuona kwa ukaribu ziwa na msitu mnene uliopo ndani na kuzunguka sakafu ya Kasoko.

 Kivutio cha Empakaai kinaweza kutembelewa wakati wowote wa majira ya mwaka, lakini inapendelewa zaidi kuanzia mwezi Juni hadi Desemba (msimu wa kiangazi).

 _Karibu Ngorongoro 

Tumerithishwa, tuwarithishe_

Post a Comment

0 Comments