DC MPOGOLO: JMAT SAIDIENI SERIKALI KUSULUHUSHA MIGOGORO YA ARDHI KWA JAMII

Mkuu  wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameitaka Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT)kwenda kushughulikia changamoto za kijamii kuisaidia Serikali kurudisha furaha na kuleta maridhiano katika ngazi za familia.

"Nendeni mkashughulikie migogoro ya kijamii kuanzia ngazi za chini za familia, kashughulikieni changamoto za mirathi, migogoro ya ardhi, migogoro ya ukatili hasa ya unyanyadaji wa kijinsia maana jamii inawahitaji sana" ameasa DC Mpogolo

Hayo ameyasema leo Januari 14,2026 katika ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa idara tatu mpya za Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania.

DC Mpogolo ameitaka JMAT kufanya kazi za maridhiano kwakuwa ni chombo ambacho Serikali kinawategemea katika kuleta maridhiano hasa katika ngazi za familia kwakuwa wao wanajukumu ya malezi katika kutatua changamoto na kero za kijamii.

Aidha Mh.Mpogolo ameiomba JMAT isichoke kushirikiana na Serikali kwasababu wananchi wanauhitaji mkubwa katika kusaidiwa kutatua changamoto zao.

Pia ameipongeza JMAT kwa kutoa elimu ya amani nchini, kutatua changamoto za kisiasa na kuleta upatanisho wa dini mbalimbali pindi inapojitokeza migogoro.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania(JMAT) Shekhe Alhad Mussa Salum amesema watahakikisha taifa hili linakuwa na amani muda wote kama walivyokabidhiwa kutoka kwa waasisi wa taifa hili likiwa salama na amani.

"Hatutakubali amani ya nchi itoweke kirahisi, tutahakikisha migogoro inapojitokeza basi sisi kama Jumuiya tutasimama kurejesha amani hiyo" Alhad Salum

Amesema JMAT wameona waongeze nguvu katika kuongeza idara tatu ikiwemo ya wazee, wanawake na vijana ili kuongeza nguvu katika kazi za marishiano nchini.

Post a Comment

0 Comments