Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini imetoa mafunzo kwa wamiliki wa huduma za malazi kuhusu; usalama, utoaji wa huduma bora kwa wateja, kufuata sheria pamoja na namna ya kujisajili katika programu tumizi iitwayo Destination Tanzania katika kipindi hiki ambacho Tanzania iko katika maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayo fanyika kuanzia mwezi Juni, 2027 kwa ushirikiano na nchi za, Kenya na Uganda.
"Wamiliki wa huduma za malazi wote katika Mkoa wa Arusha wanapaswa kuwa tayari kutoa huduma zitakazowafanya wageni watakao kuja wakati wa mashindano ya AFCON 2027 kuwa na kumbukumbu ya kudumu na kuwa na shauku ya kurudi tena baada ya mashindao kuisha,” amesema, Bi. Kunzugala.
Mafunzo hayo kwa watoa huduma za malazi katika Mkoa wa Arusha yamefanyika leo katika ukumbi wa Chuo cha Fedha Arusha (IAA) na kuhudhuriwa na wamiliki wa huduma za malazi yaani AirBnB, Homestays, Hoteli, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), na Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kamati ya Maandalizi ya AFCON 2027, anayehusika na malazi, usafiri na ufasiri wa lugha, Bw. Allen Alex, amebainisha kuwa wageni wapatao milioni 1.8 wanatazamiwa kuja Afrika Mashari kushiriki mashindano ya AFCON 2027 na angalau watu laki 5 mpaka 6 wataweka makazi yao nchini Tanzania. Hivyo wamiliki wa huduma za malazi wanapaswa kuwa tayari kuwakarimu wageni hao ili waweze kuwa na kumbukumbu ya kudumu kuhusu Tanzania.
“Ninyi watoa huduma za malazi ndio ambao mtasababisha wageni waiseme Tanzania vizuri au vibaya, waendelee kuwepo na kutamani kurudi au wasirudi. Wageni wataamua hayo kutokana na namna mtakavyowahudumia na ukarimu wenu kwao,” amesisitiza Alex.
Mafunzo hayo kwa watoa huduma za malazi ni moja ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii katika kukamilisha maandalizi ya kupokea wageni watakaohudhuria mashindano ya AFCON 2027, huku ikilenga kutumia mashindano hiyo kutangaza vivutio vya utalii, kuongeza idadi ya watalii na kukuza mapato yatokanayo na shughuli za utalii nchini.




0 Comments