Serikali imesema itaendelea kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU), kwa kuboresha vituo vya huduma, kuwezesha vikundi na kuimarisha ushirikiano na wadau, ili kuhakikisha Tanzania inafikia lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dk. Jim Yonazi, wakati wa ziara yake mkoani Shinyanga, ambapo alitembelea vikundi mbalimbali vya vijana vinaoishi na Maambukizi ya VVU pamoja na Kituo cha Maarifa Kahama kilichopo Kagongwa mkoani humo.
Dk. Yonazi amesema juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau zimeanza kuzaa matunda, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utoaji wa elimu, upimaji, ushauri nasaha, pamoja na huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.
Dk. Yonazi amesema juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau zimeanza kuzaa matunda, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi katika utoaji wa elimu, upimaji, ushauri nasaha, pamoja na huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.
“Lengo ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu nao, lakini vilevile wanapata elimu inayowasaidia katika mapambano dhidi ya UKIMWI na maambukizi ya UKIMWIi,” amesema.
Amesema Serikali imeendelea kuboresha huduma hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa wakati, huku akiwataka wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha afua za kukabiliana na VVU.
Dkt. Yonazi amepongeza Mkoa wa Shinyanga kwa kufikia malengo ya kimataifa ya 95-95-95, akisema hatua hiyo ni ishara ya mafanikio katika jitihada za kupunguza maambukizi mapya na madhara yatokanayo na VVU.
“Serikali imeamua kwa makusudi kabisa kuongeza nguvu yake. Ndiyo maana imeanzisha Mfuko wa Mfadhili, na asilimia 70 ya fedha hiyo inakwenda katika Mfuko wa UKIMWI ili kusaidia afua mbalimbali na kuondokana na utegemezi,” amesema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,Mhe. Mbona Mahita, alisema mkoa huo bado una kiwango cha maambukizi ya VVU kilicho juu ya wastani wa kitaifa, ambapo Shinyanga ina asilimia 5.6 ikilinganishwa na asilimia 4.4 ya kitaifa.Mahita alisema Serikali imeendelea kuongeza elimu kuhusu VVU katika ngazi mbalimbali, kuanzia kaya hadi jamii, ili wananchi wawe na uelewa wa kutosha kuhusu namna ya kujikinga na maambukizi.
“Shinyanga ni business hub kwa Kanda ya Ziwa. Movement za watu mara kwa mara ni kubwa. Watu wanaoingia na kutoka ni wengi, ndiyo maana tumeshuka mpaka kwenye ngazi za kijamii katika utoaji wa elimu,” alisema.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk. Honoratha Rutatinisibwa, alisema mkoa huo una vituo 374 vinavyotoa huduma za afya, ambapo vituo 120, sawa na asilimia 32, vinatoa huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.
Dkt. Rutatinisibwa amesema, kwa mujibu wa utafiti wa maambukizi ya VVU uliofanyika mwaka 2023, kiwango cha maambukizi mkoani Shinyanga ni asilimia 5.6, ikilinganishwa na wastani wa kitaifa wa asilimia 4.4.
Akizungumzia huduma zinazotolewa katika Kituo cha Maarifa Kahama kilichopo Kagongwa, Mratibu wa Kudhibiti Maambukizi ya VVU, Homa ya Ini na Magonjwa ya Ngono Kahama, Dkt. Herry Silvester, amesema kituo hicho kinatoa huduma za tiba na matunzo, pamoja na huduma maalumu kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi.






0 Comments