Itilima, Simiyu
Vikundi vya kijamii vinavyotekeleza matengenezo ya kawaida ya barabara kupitia Mpango wa CBRM unaotekelezwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) vimetakiwa kushirikiana na wananchi katika kulinda na kutunza miundombinu ya barabara ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Itilima Mhe. Anna Gidarya wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha jumla ya vikundi 16 kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kutekeleza kwa ufanisi shughuli za matengenezo madogo madogo ya barabara katika maeneo yao.
Aidha, amevipongeza vikundi hivyo kwa kupata fursa ya kushiriki moja kwa moja katika matengenezo ya barabara akieleza kuwa hatua hiyo si tu inasaidia kuboresha miundombinu bali pia inawapa wananchi nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya maeneo yao.
Mhe. Gidarya pia amewataka wanavikundi kuwa na umoja, mshikamano na ushirikiano huku wakiepuka migogoro na changamoto za ndani zinazoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru TARURA kwa kuwajengea uwezo kuhusu utekelezaji wa matengenezo ya kawaida ya barabara ambapo wameahidi kutumia maarifa waliyoyapata kuwa mabalozi wa utunzaji wa miundombinu pamoja na kuimarisha umoja na mshikamano ndani ya vikundi vyao.
Wamesema watahakikisha manufaa yanayotokana na ushiriki wao katika mpango huo yanatumika kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja, vikundi na jamii kwa ujumla.




0 Comments