WATAALAMU WA MAABARA TOENI MAJIBU SAHIHI KUWASAIDIA WATANZANIA - DKT. BITEKO


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko.

(Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati)

Naibu Waziri Mkuu wa Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Wataalam wa Maabara za binadamu nchini kuionea wivu taaluma yao kwa kuwa ina mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 2, 2024 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Kongamano la 37 la Kisayansi la Wataalamu wa Maabara za Afya nchini na Kongamano la 23 la Kisayansi la HUOQAS na Mkutano Mkuu wa Mwaka.

Wito wangu kwenu ioneeni wivu, muipende na kuithamini taaluma yenu, msikae pembeni mnapoona kuna changamoto semeni bila kuogopa. Wataalamu wa Maabara bila ninyi tiba haiwezi kufanyika na mfanye kila mtu awaheshimu,” amesema Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko amesisitiza “ Nataka niwaambie mnapofanya kazi hii mnawahudumia Watanzania tufanye kwa upendo na tuwape majibu sahihi ili kuisaidia Serikali yetu kuwa mhudumu wa kweli wa wananchi.”

Aidha, Dkt. Biteko ameelekeza waajiri nchini kuruhusu watumishi wao wa kada ya maabara kushiriki katika makongamano ya kitaaluma huku akiwataka washiriki  kujifunza kupitia mada zitakazowasilishwa na baadaye kuwashirikisha wataalam wenzao ambao hawakuhudhuria.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itafanyia kazi  changamoto zote zilizowasiliahwa na MeLSET.

“Changamoto zote nimezichukua na naitaka Wizara kuchukua hotuba ya MeLSAT na kuzifanyia kazi changamoto zote zilizowasilishwa katika mkutano  ili mwaka ujao changamoto zisiwe hizi tuwe na masuala mengine ya kuzungumza,” ameeleza Dkt. Biteko.

Naye, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye sekta ya afya na hiyo inaonesha hatua kubwa imepigwa huku akitaja shilingi trilioni 1.2 zilizotumika kuboresha maabara za afya nchini.

Ametaja eneo lingine lililoboreshwa katika sekta hiyo ni vitendea kazi  vya kiuchunguzi kwa uwepo wa vifaa vya kisasa zikiwemo  mashine 13 za MRI Digital xray 346, ulta sound 476 na ufundishaji wa ubingwa bobezi.

“ Maboresho hayo yamegusa pia Mfuko wa ufadhili wa Rais Samia ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu pekee umeshagharamia kiasi shilingi bilioni 9 ili kusomesha wataalamu wa sekta ya afya hapa nchini. Tumetanua wigo wa utalii wa afya kupitia uwekezaji huu uliofanywa na Mhe. Rais Samia.” Amesisitiza Mhe. Mhagama.

Kaimu Mganda Mkuu wa Serikali, Dkt. Saitore Laizer  amesema kuwa Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kukuza vyama mbalimbali vya kitaaluma  ili viweze kusaidia kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali yanayolenga kuimarisha sekta ya afya nchini.

Amebainisha kuwa baada  ya Serikali kuwekeza katika vifaa tiba na miundombinu pamoja na watumishi suala kubwa  ni kuhakikisha kuna ubora wa huduma za afya na kuwa hicho ni kipaumbele ili  mambo yote  yaliyofanyika yaweze kuwa na tija.

Suala la usugu wa vimelea vinaweza kuhama kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kama yalivyo magonjwa na ikifika huko maana yake tunaweza kupoteza maisha na gharama kubwa. Aidha, hakuna huduma bora za tiba bila ya huduma bora za uchunguzi na ndio maana kuanzia mwaka jana Serikali imeanza kutoa ufadhili wa masomi kwa kusomesha wataalamu wa maabara katika ngazi za kati katika vyuo vya umma, binafsi na mashirika ya dini hii inaonesha dhamira ya Serikali katika kuendelea kuimarisha sekta hii muhimu.” Amesema Dkt. Laizer.

Rais wa Chama Cha Wataalam wa Maabara za Afya Tanzania (MeLSAT), Bw. Yahya Mnung’a amesema  kuwa lengo la Kongamano hilo ni kuwakutanisha  wataalam na kutatua changamoto za kitaaluma katika maabara za binaadamu pamoja na uwepo wa maonesho ya vifaa vinavyotumika katika maabara za binadamu.

Ameongeza kuwa wataalamu hao wataendelea kutoa huduma kwa Watanzania licha ya uwepo wao kwa idadi ndogo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wataalamu wa Maabara za Afya Afrika (FeLPA), Bw. Mulate Mubanga amesema kuwa idadi kubwa ya watu hupata madhara kwa kutumia dawa bila kufanya vipomo vya maabara na kuwa ni vyema Serikali barani Afrika  pamoja na wadau wa sekta hiyo kupatia ufumbuzi changamoto hiyo.

“ Naipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa na idadi kubwa ya maabara pamoja na uwekezaji mkubwa uliofanya katika maabara, aidha elimu kuhusu matumizi ya dawa itolewe kwa wananchi ili kupunguza usugu wa dawa . Tunatumaini Serikali na wadau itaendelea kutoa elimu ya matumizi ya dawa kwa faida ya kizazi kijacho. Amesema Bw. Mubanga.

Post a Comment

0 Comments