Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Chama cha Riadha Mkoa wa Dar es Salaam(DAA), kimeweka mikakati ya kupambana na matumizi ya dawa zisizoruhusiwa michezoni kwa kuandaa kliniki maalumu ya kutoa elimu kwa wachezaji, makocha na wadau wengine wa michezo.
Kliniki hiyo inatarajiwa kufanyika Desemba 10 na 11 mwaka huu, ikiendeshwa na Mtaalamu kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Halima Bushiri, ikiwezeshwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uelewa kuhusu madhara ya matumizi ya dawa hizo.
Akizungumzia maandalizi hayo, Makamu wa Mwenyekiti wa DAA, Mwalimu Elizabeth Tungaraza, amesema chama kiliona umuhimu wa kutoa elimu hiyo kwa wadau wa michezo, lakini kilikabiliwa na changamoto ya uwezo wa kugharamia shughuli hiyo, hivyo kuamua kutafuta wadau wa kukisaidia kufanikisha mpango huo.
Alisema kupitia juhudi hizo, walifanikiwa kupata ushirikiano wa BoT, ambayo imetambua umuhimu wa elimu hiyo na kukubali kusaidia kufanikisha kliniki hiyo.
"Matumizi ya dawa zisizoruhusiwa si jambo dogo, kwani yanadhalilisha taifa, kurudisha nyuma maendeleo ya wanamichezo na kuondoa uaminifu katika michezo," amesema.
Amebainisha kuwa, mwanamichezo anayebainika kutumia dawa hizo anaweza kunyang'anywa medali aliyoipata, jambo linaloweza kulisababishia taifa fedheha na kuharibu taswira ya michezo yake kitaifa na kimataifa.
Amebainisha, kliniki hiyo itahusisha wanamichezo, makocha, mameneja, mawakala, waamuzi na wanahabari, ambao wanapaswa kupata elimu kuhusu dawa zinazopigwa marufuku na madhara yake ili waweze kusaidia kuifikisha kwa jamii.
Katika hatua nyingine, Chama hicho kinatarajiwa kufanya kikao cha Kamati Tendaji Novemba 24 mwaka huu, kwa lengo la kutathmini mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika kipindi cha mwaka mmoja tangu viongozi wa sasa kuingia madarakani.
Tungaraza, amesema kikao hicho kitafanyika katika ofisi za chama na kujadili utekelezaji wa shughuli mbalimbali, kubaini maeneo ambayo hayajafikiwa na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji katika mwaka ujao.
Ameongeza kuwa, chama hicho kinatarajiwa kufanya mkutano mkuu wa mwaka Desemba Mosi mwaka huu, ambao pamoja na kujadili ripoti ya mwaka, utapitisha bajeti ya mwaka 2027.
Kwa upande wake, Katibu wa DAA Felix Chunga, amesema Mkoa wa Dar es Salaam unatarajiwa kushiriki mashindano ya Ladies First ambayo yatafanyika Novemba 27 hadi 29 mwaka huu viwanja vya Filbert Bayi Schools (FBS), Kibaha kwa Mathias mkoani Pwani.
Alisema chama kimejipanga kutekeleza shughuli mbalimbali za kujenga hamasa na kuwafahamisha wadau kuhusu mipango yake, huku akisisitiza umuhimu wa kupata ushirikiano wa wadau ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

0 Comments