WASANII WAOMBA KUPUNGUZIWA KODI KWENYE VIFAA VYA MUZIKI


Msanii wa muziki wa kizazi kipya kutoka Kundi la Weusi Nick wa Pili (Kushoto) akisisitizajambo wakati akiongea na wadau wa Sanaa (hawako pichani) kwenye programu ya Jukwaa la Sanaa inayofanyika kwa mwezi mara mbili siku ya Jumatatu makao makuu ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam. Wengine kushoto kwake ni wasanii wanaounda kundi hilo John Simon aka Joh Makini na G Nako na Afisa kutoka BASATA  Elineca Ndowo. 

Na Mwandishi Wetu,Basata

Baadhi ya wasanii nchini wameiomba Serikali kupitia Wizara ya Fedha kufikiria kupunguza au kufuta kabisa ushuru wa forodha unaotozwa kwenye vifaa vya muziki wanavyoagiza kutoka nje ili kukuza Sanaa na kusaidia mamilioni ya vijana ambao wamejiajiri kupitia sekta hiyo.

Akizungumza kwa niaba ya wasanii mapema wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa la Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) mmoja wa wasanii anayeunda kundi la muziki wa kizazi kipya la Weusi Nick wa Pili alisema kwamba, kwa sasa sekta hiyo ni kimbilio la ajira kwa vijana wengi kwa hiyo Serikali haina budi kupunguza kodi kwa zana mbalimbali zinazotumiwa na wasanii ili kurahisisha uzalishaji, kukuza tija na uchumi.

“Wasanii wengi kwa sasa wanakwenda kufanya video na kutengeneza muziki nje ya nchi. Hii inatokana na teknolojia yetu kuwa chini ya wenzetu. Naamini Serikali ikipunguza kodi katika vifaa hivi na kuwawezesha wataalam tulionao basi nchi zote jirani zitakimbilia kwetu” alisema Nick.

Aliongeza kwamba vipaji vya wasanii vipo vingi lakini kutokana na uzalishaji duni wa kazi za muziki na hata filamu wasanii wamejikuta wakishindwa kushindana ipasavyo nje ya nchi na mara nyingi kutumia gharama kubwa katika kufuata teknolojia hizo za juu nchi za nje na hivyo kuikosesha serikali mapato.

“Wasanii wanakwenda kulipa zaidi ya milioni arobaini kwa video moja tu nje ya nchi, hizi fedha zinakwenda kukuza uchumi wa nchi zingine. Naamini kama Serikali ikijenga mazingira mazuri ya kiteknolojia na zaidi kushusha gharama hizi basi nchi yetu itafaidika zaidi na Sanaa” alisisitiza .

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mitaji na Misaada kwa wasanii kutoka BASATA Bi. Elineca Ndowo alisema kwamba sekta ya Sanaa nchini inazidi kukua na hivyo lazima wasanii nao wafikirie kufanya kazi kisasa na kwa kufuata taratibu zote ili kuipa serikali uhakika katika kupanga kulingana na hali halisi.

“Sekta ya Sanaa inakua, lazima tuisaidie Serikali kuipa takwimu sahihi na moja ya njia ya kuhakikisha hili ni kwa wasanii kujisajili, kusajili kazi zao na kuhakikisha taarifa sahihi na kwa wakati zinapatikana. Hili litarahisisha upangaji wa mipango” alisema Bi. Ndowo.


Jukwaa la Sanaa la BASATA ni programu ambayo hufanyika kwa mwezi mara mbili siku ya Jumatatu na hutumika kama jamvi la kuwaelimisha wasanii na kuwakutanisha kwa pamoja katika kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo sekta yao.  

Post a Comment

0 Comments