RAS MKOA WA PWANI AFUNGUA MAFUNZO YA O&OD



Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, amefungua kikao kazi cha mafunzo ya siku mbili kwa vikosi kazi vya utekelezaji wa Mfumo wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD) ulioboreshwa, Vikosi kazi hivyo vimejumuisha wataalamu mbalimbali wa ngazi ya Mkoa na Halmashauri, 

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, kilichofanyika leo Januari 15, 2026. katika ukumbi wa mikutano uliopo ofisi ya Mkuu wa MKoa wa Pwani, Mnyema amewasisitiza watalaam hao kuhakikisha wanasikiliza kwa makini mafuzno hayo ili kuweza kuongeza ufanisi katika kuingiza kazi na taarifa kwa usahihi ili kuwezesha Mkoa kutekeleza mfumo huo ipasavyo.

Aidha aliongeza kuwa mafunzo hayo si ya mzaha bali ni muhimu katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Serikali kwa maslahi ya wananchi. Amesisitiza kuwa Mkoa wa Pwani unaongoza katika maeneo mbalimbali, hivyo ni wajibu wa watalaam hao kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo bila visingizio.

“Baada ya mafunzo haya nataka kuona mabadiliko yanayoonyesha mkoa au wizara inakwendaje. Haikubaliki kushindwa kutimiza majukumu yetu,” amesema Mnyema.

Ameongeza kuwa Serikali inataka wananchi waone miradi yao ikitekelezwa kwa vitendo na inayotekeleza vipaumbele vyao, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa sahihi na kuepuka tabia ya “kupika taarifa”. Pia amekumbusha kuwa utekelezaji wa mfumo wa O&OD unapaswa kuzingatia kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, inayosisitiza kutokukubali katika kushindwa.

“Maeneo yenye changamoto tumefundishwa Twende tukayafanyia kazi, Mfumo huu unatusaidia kupanga na kutekeleza miradi kulingana na vipaumbele vya wananchi na hapa tumekula kiapo cha uadilifu, hivyo yeyote atakayekiuka maelekezo na taratibu atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.,” amefafanua Mnyema.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, Grace Tete, amesema baada ya mafunzo hayo mkoa unatarajia kuongeza kiwango cha utekelezaji wa mfumo wa O&OD ulioboreshwa pamoja na kuwa na mpango bora wa bajeti unaozingatia jitihada na mahitaji ya jamii.

Pia Tete ameongeza kuwa awali mkoa ulikuwa na changamoto ya uelewa mdogo wa mfumo huo, hususan kwa vikosi kazi vya ngazi ya mkoa na halmashauri kutofahamu vizuri viashiria vya O&OD ulioboreshwa vilivyowekwa katika Mfumo wa IMES na namna ya kuviingiza katika mfumo huo. Hata hivyo, amesema baada ya mafunzo hayo, mkoa unatarajia kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji na ufuatiliaji wa mipango ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments