TAMASHA LA PASAKA LARUDI KWA KISHINDO 2026


 Tamasha la Pasaka, linaloandaliwa na kuratibiwa na Msama Promotions, limeendelea kuwa tukio muhimu la muziki wa Injili nchini Tanzania. Kwa msimu huu, tamasha hilo linatarajiwa kufanyika katika mikoa 20, likianzia jiji la Dar es Salaam, na kuwaleta pamoja wasanii nguli wa nyimbo za Injili kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, alisema kuwa msimu huu wa Pasaka Tamasha hilo litaanza tarehe 5 Aprili 2026, na lengo lake ni kutoa burudani kwa waumini wa dini ya Kikristo na pia kwa wale wasio wa Kikristo, sambamba na kusambaza ujumbe wa kiroho.

“Wasanii wakubwa watapanda majukwaa katika mikoa yote 20 kutoa burudani kabambe. Hii ni dhamira yetu kama waandaji kuwapa watanzania burudani ya hali ya juu kupitia muziki wa Injili,” alisema Msama.

Historia ya Tamasha la Pasaka imepambwa na uhai wa waimbaji maarufu kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya. Baadhi ya wasanii waliofanya vizuri katika matamasha ya Pasaka ya awali ni pamoja na mwimbaji bora kutoka Afrika Kusini. Msama alisema kuwa msimu huu wa 2026, wasanii kutoka nje ya nchi wataleta chachu ya kipekee, ikiwa ni mwendelezo wa matamasha ya Pasaka ya awali ambayo yalivutia hadhira kubwa.

Kwa mujibu wa Msama, tamasha hili litakuwa la kishindo na lenye kutoa ujumbe wa kiroho, huku likiwa na lengo la kuwaleta pamoja Watanzania na kueneza ujumbe wa matumaini na shukrani kwa Mungu.

Ingawa tamasha hili hufanyika kila mwaka, kwa kipindi cha hivi karibuni halikufanyika. Mwaka huu 2026, Tamasha la Pasaka limepangwa kurejea kwa nguvu zote, likitarajiwa kuwa tukio la kihistoria kwa waimbaji na mashabiki wa muziki wa Injili.

Post a Comment

0 Comments