WIZARA ya Habari
Utamaduni na Michezo imeliagiza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutoa adhabu
kwa timu ya Ruvu Shooting kutokana na kitendo cha ubaguzi kilichofanywa na
wachezaji wa timu hiyo dhidi ya mshambuliaji wa Yanga kutoka nchini Rwanda,
Hamis Tambwe.
Akizungumza na Ripota wa
Globu ya Jamii, Naibu Waziri wa Habari, Juma Nkamia amesema kuwa TFF isikae
kimya kutokana na matamshi ya udhalilishaji juu ya Tambwe na kuiagiza TFF
kuchukua hatua za kinidhamu haraka iwapo itathidibitika mshambuliaji huyo alitolewa
maneno hayo ya udhalilishaji ili iwe fundisho kwa wengine.
"Hakuna nchi yoyote
duniani inayopenda vitendo vya ubaguzi, kitendo ambacho upendi kufanyiwa
usimfanyie mwenzie, nimesikia malalamiko ya Tambwe kama ni kweli Ruvu Shooting
wamemuita mkimbiza wajue sio kitu kizuri tena wale ni jeshi, nadhani wanajua
madhara ya vita.
"Wenzetu Burundi
hawakupenda kuingia vitani, hakuna nchi yoyote inayopenda kuwa vitani, vita ni
mbaya hata hapa inaweza kutokea, ni jambo la kumshukuru Mungu mpaka leo mna amani,
uwezi kujua mtu unayemwambia ameumia kiasi gani na hiyo vita ni ndugu wangapi
au marafiki wangapi amewapoteza sio kitu kizuri, naiagiza TFF ishugulikie suala
hili kwa kuchukua hatua za haraka."alisisitiza Nkamia.
Kauli ya Nkamia imekuja
siku moja baada ya Tambwe kulalamikia kitendo cha kuitwa mkimbizi na wachezaji
wa Ruvu Shooting wakiongozwa na George Michael ikiwa ni pamoja na kumkaba
nusura wamtoe roho.
"Maneno makali
waliyonitamkia yananiuma sana roho hadi sasa, wameniita mkimbizi, eti nimekimbia
vita nyumbani Burundi, vita hata hapa inaweza kutokea, hakuna anayependa mabaya
kama hayo yatokee, kumwambia mtu haujui kapoteza ndugu wangapi, si sahihi
kabisa, cha kushangaza wale ni wanajeshi lakini hawaonyeshi kuwa wanajua athari
za vita." kauli iliyotolewa na Tambwe jana.
Hata hivyo Chama cha
Waamuzi nchini (FRAT), kimetangaza kumfungia mwamuzi wa kati wa mchezo huo
Mohamed Theofil, huku ikiwaweka kwenye uchunguzi waamuzi wasaidizi Michael
Mkongwa na Yusuf Sekile.
Mwenyekiti wa FRAT, Salum
Chama aliiambia Globu ya Jamii kuwa wamefikia uamuzi wa kumsimamisha Theofil
baada ya ripoti ya Kamisaa kuonyesha kuna mapungufu yaliyofanywa na mwamuzi
huyo ambaye katika mchezo huo uliomalizika kwa suluhu, alishindwa kumudu mchezo
kutokana na rafu za mara kwa mara kitendo kilicholazimu mpira kusimama kila
dakika.
"Ripoti ya kamisaa
imeonyesha kuna udhaifu mkubwa uliofanywa na mwamuzi, kamati yangu imemfungia
kupisha uchunguzi, na bado tunaendelea na uchunguzi pia kwa waamuzi wasaidizi,
kikao cha kamati yangu kitakaa Februari 6 kuwajadili na kuangalia adhabu
stahiki itakayofaa.
"Kitendo
kinacholalamikiwa sana ni kile cha Tambwe, na ni kweli kila mtu ameona, hata
kama ripoti ya kamisaa isingesema tungechukua hatua kwa sababu wapo viongozi wa
TFF walioona, tunachunguza ripoti ya mechi asesa, kamisaa,"alisema Chama.
Hata hivyo, Chama alisema kuwa hawafanyi kazi kwa shinikizo la
Yanga ambao waliwapa mpaka Jumamosi wawe wameshatoa adhabu kwa waamuzi wa
mchezo wao na Ruvu Shooting la sivyo watagomea Ligi.Habari chanzo Globu ya Jamii WWW.Michuzi.BLOGSPOT.COM
0 Comments