MADIWANI MKOA WA PWANI WATAKIWA KUWA WABUNIFU KUKUZA UWEKEZAJI


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ametoa wito kwa Madiwani wapya kuwa wabunifu na kuvutia wawekezaji ikiwa ni katika kukuza uchumi wa Mkoa .

Aidha Madiwani hao wametakiwa kufahamu vipambele vya Mkoa wa Pwani na kuhumili ushindani wa kiuchumi hasa katika ngazi ya Kimataifa pamoja na kuwa wabunifu katika kubuni mbinu mpya na za kuvutia wawekezaji. 

"Kwakuwa ninyi ni Madiwani wageni japo wengine wamerudi na lakini wote mnatakiwa kufahamu vipaumbele vya Mkoa wa Pwani ambavyo mkivifuata vitaleta tija zaidi kwenye uwekezaji wa viwanda ,pia mnapaswa kufahamu muelekeo wa uchumi wa dunia ulivyo hivi sasa kwa sababu tunazungumzia ushindani wa kiuchumi na vita za kiuchumi katika ngazi za Kimataifa" amesema
Kunenge.

RC Kunenge amesema hayo leo tarehe 8, Januari,2026 alipozungumza katika kikao kazi kilichofanyika Wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na Wakuu wa Wilaya zote, Meya wa Manispaa ya Kibaha, Wenyeviti wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani, Makatibu Tawala wote , Wakuu wa Idara na Wataalamu mbalimbali. 

Wakati huohuo RC Kunenge amesisitiza Hospitali zote za Wilaya Mkoa wa Pwani kusimamia matumizi ya Telemedisini katika Hospitali zote Mkoani hapa kwani teknolojia imerahisisha mambo mengi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani  Abubakari Kunenge, amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kuzingatia taratibu za kiutendaji na kuheshimu mihimili ya nchi Mahakama, Serikali, na Bunge ambapo pia ameongeza kwa kusema kuwa ni muhimu kwa watendaji na Madiwani wapya kuelewa misingi ya Utawala wa Sheria ili kuepuka kufanya maamuzi yanayoingilia mamlaka nyingine bila kufuata utaratibu uliowekwa.
 
Baadhi ya washiriki wameipongeza hatua hiyo ya Nkoa wakisema imewapa dira mpya. Wamesema kikao hicho kimewakumbusha namna bora ya kuongoza na kutekeleza vipaumbele vya mkoa, jambo ambalo linaenda sambamba na kasi ya utendaji pamoja na ahadi za siku 100 za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

 Viongozi hao wamepata nafasi ya kuchambua picha halisi ya hali ya uchumi duniani na kitaifa, huku kila Halmashauri ikitakiwa kutathmini mchango wake katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Pwani.

Post a Comment

0 Comments