MFALME ABDULLAH BIN ABDUL- AZIZ KUZIKWA LEO BAADA YA SALATUL JUMAA,SAUDIA ARABIA


MFALME Abdullah bin Abdul-Aziz wa Saudia (pichani) aliyefariki usiku wa kuamkia leo anatarajiwa kuzikwa leo baada ya swala ya Ijumaa. Taarifa iliyotangazwa na televisheni ya nchi hiyo imesema kuwa, uongozi umechukuliwa na Salman bin Abdulaziz ndugu wa Abdullah. 

Mfalme huyo aliyekuwa anakaribia umri wa miaka 90 alipelekwa katika hospitali moja ya mjini Riyadh mwanzoni mwa mwezi huu kwa ajili ya matibabu baada ya hali yake ya kiafya kuzorota ambapo alikuwa na matatizo katika mfumo wa upumuaji. 

Habari zinasema kuwa, Mfalme Abdullah amefariki dunia saa saba za usiku wa kuamkia leo kwa majira ya Saudia. Ofisi ya ufalme ya nchi hiyo imetangaza kuwa, sala ya maiti itasaliwa baada ya sala ya alasiri ya leo katika chuo cha Imam Turki bin Abdullah mjini Riyadh. 

Aidha habari zimeongeza kuwa, Salman bin Abdulaziz Aal Saud amepata baiya ya kuwa mfalme kwa mujibu wa katiba ya utawala wa Saudi Arabia ambapo naye amemteua Muqrin bin Abdul-Aziz, ndugu wa baba mmoja wa Mfalme Abdullah kuwa mrithi wa kiti cha ufalme baada yake. 

Mfalme Abdullah aliyezaliwa mjini Riyadh, alikuwa mtoto wa 13 wa mfalme Abdul-Aziz, mwasisi wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo. Baadhi ya duru zinasema kuwa, bado kuna mivutano ya kuwania madaraka kati ya watu wa ukoo wa Aal Saud.innalilah wainna ilaih rajiun

Post a Comment

0 Comments