
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na utenguzi wa viongozi mbalimbali wa serikali, hatua inayolenga kuimarisha ufanisi wa utendaji kazi katika ngazi za juu za uongozi wa nchi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 8, 2026 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, uteuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka.
Katika uteuzi huo, Mhe. Patrobas Paschal Katambi (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, akichukua nafasi ya Mhe. Boniface George Simbachawene (Mb.) ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Kabla ya uteuzi huo, Mhe. Katambi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.
Aidha, Mhe. Prof. Palamagamba John Aidan Kabudi (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Ikulu (Kazi Maalum), akitoka katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Katika mabadiliko mengine, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb.) ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, akipandishwa kutoka nafasi ya Naibu Waziri katika wizara hiyo.
Rais Samia pia amemteua Mhe. Dennis Lazaro Londo (Mb.) kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, nafasi aliyochukua kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambako alikuwa Naibu Waziri.
Kwa upande wa Naibu Mawaziri, Mhe. Ayoub Mohamed Mahmoud (Mb.) ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika ngazi ya makatibu wakuu, Dkt. Richard Stanslaus Muyungi ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), akichukua nafasi ya Mheshimiwa Cyprian John Luhemeja aliyeteuliwa kuwa Balozi.
Rais Samia pia amewateua Mhandisi Zena Ahmed Said, Bw. Waziri Rajab Salum pamoja na Meja Jenerali Mbaraka Naziad Mkeremy kuwa Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, Mhandisi Ally Samaje ameteuliwa kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), akichukua nafasi ya Dkt. Mussa Daniel Budeba.
Katika hatua nyingine, uteuzi wa Prof. Eliakimu Mnkondo Zahabu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) umetenguliwa.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa viongozi wote walioteuliwa wataapishwa rasmi tarehe 13 Januari, 2026, katika Ikulu ya Chamwino, Dodoma kuanzia saa 8.00 mchana.
Mabadiliko hayo yanaonesha dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha utendaji kazi wa serikali na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.


0 Comments