Ndugu Wananchi,
Naomba sote tumshukuru Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma kwa kutuwezesha kuzungumza tena mwisho wa mwezi huu. Katika mwezi tunaoumaliza leo taifa letu lilipata msukosuko mkubwa kufuatia mgomo wa madaktari. Nashukuru mgomo huo umeisha lakini makovu yake yatabaki maisha katika kumbukumbu za historia ya taaluma ya tiba hapa nchini.
Leo, Mheshimiwa Waziri Mkuu amenipa taarifa kuwa Kamati aliyounda kushughulikia madai ya madaktari imekamilisha kazi yake na kuwasilisha taarifa yake kwake. Kuanzia kesho Serikali itaifanyia kazi taarifa hiyo na kuamua ipasavyo kulingana na uwezo uliopo. Nawaomba ndugu zetu madakatari kuwa na moyo wa subira. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia ndugu zetu madaktari na watumishi wengine wote wa sekta ya afya kwamba Serikali inatambua, inajali na kuthamini kazi wazifanyazo na mchango wao katika kulinda na kudumisha afya za wananchi wa Tanzania. Aidha, narudia kutoa pole
zangu za dhati kwa wananchi na hasa wagonjwa nchini kwa mateso waliyoyapata katika kipindi cha mgomo. Ni matumaini yangu kuwa hali kama ile haitajirudia tena katika nchi yetu.
Ndugu Wananchi,
Tukio lingine la kusikitisha ni mauaji ya Songea. Yapo yale yanayohusishwa na imani za ushirikina, na yapo yale ambayo yalitokea kwenye maandamano. Napenda kutumia nafasi hii kuelezea masikitiko yangu kwa vifo hivyo na kutoa pole na rambirambi zangu na za wananchi wa Tanzania kwa ndugu wa marehemu wetu hao. Tupo pamoja nanyi katika misiba hii mikubwa na majonzi. Napenda kuwahakikishia wananchi wa Songea kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya usalama imekuwa inafanya na itaendelea kufanya uchunguzi wa kina wa mauaji haya mpaka wahusika wote wapatikane na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Nimearifiwa kuwa, mpaka sasa kwa mauaji 13 yanayohusishwa na imani za ushirikina watuhumiwa 26 wamekwishakamatwa. Na kwa mauaji yaliyotokana na maandamano, askari polisi wanne wamekamatwa na upelelezi unaendelea.
Ndugu Wananchi;
Nashukuru kwamba amani na utulivu vimerejea katika Manispaa ya Songea. Nawapongeza sana viongozi wa ngazi zote na wananchi kwa ujumla kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuwezesha usalama na utulivu kupatikana. Tafadhali endeleeni na juhudi hizo mpaka mambo yatengemae kabisa.
Ndugu Wananchi;
Katika mwezi huu pia, Bunge letu Tukufu lilifanya mkutano wake wa sita na miongoni mwa maamuzi makubwa yaliyofanywa ni kupitisha Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011 hususan kuhusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba ya nchi. Nimekwishatia saini marekebisho hayo tarehe 20 Februari, 2012 na hivyo sasa yako tayari kutumika.
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi kwa Wabunge wetu kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya ya kupitisha marekebisho hayo.
Aidha, natoa pongezi maalum kwa vyama vya siasa vya CCM, CHADEMA, CUF na NCCR - Mageuzi pamoja na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali kwa maoni na mapendekezo yao ambayo ndiyo yalikuwa chachu ya marekebisho yaliyofanyika. Pia, nawashukuru kwa ushirikiano wao uliowezesha mafanikio kupatikana.
Tulipotoka
Ndugu Wananchi;
Bila ya shaka mtakumbuka kuwa baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Sheria ya Mabadikiko ya Katiba tarehe 18 Novemba, 2011, kulikuwepo na maneno mengi na maoni mbalimbali katika jamii. Wapo baadhi ya wadau hasa baadhi ya vyama vya siasa na asasi za kiraia ambao waliniomba nisitie sahihi Muswada huo kuwa Sheria na badala yake niagize Bunge liuzungumze upya. Aidha, vyama vya siasa vya CHADEMA, CUF na NCCR – Mageuzi na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali waliomba kukutana nami tuzungumzie mchakato mzima wa Katiba. Sikusita kuwakubalia na kwa nyakati mbalimbali tulikutana na kuzungumza nao.
Ndugu Wananchi;
Katika mazungumzo yangu nao niliwaeleza ugumu niliouona kuhusu kuacha kutia sahihi Muswada huo na kuurudisha tena Bungeni kujadiliwa upya. Nilichelea kuliingiza taifa letu katika mgogoro mkubwa wa kisiasa na kikatiba usiokuwa na lazima. Mgogoro ambao tunaweza kuuepuka kwa kutumia njia nyingine za kikatiba na kisheria kufikia malengo yale yale. Kitendo cha mimi kukataa kutia sahihi kingejenga chuki kwa upande wa Wabunge walio wengi ambao waliujadili Muswada na kuupitisha. Wengeweza kuhisi wamedharauliwa na kuonekana hawana thamani.
Katika mazingira hayo mtakapowarudishia Muswada huo kuujadili kuna hatari ya kutokupata ushirikiano wao na kushindwa kupata kile kinachotarajiwa. Wanaweza kujadili na kuamua kukataa mapendekezo yote mapya na kubakia na msimamo wao ule ule.
Ndugu Wananchi;
Kwa ajili hiyo, busara ilinielekeza kuwa tusitumie njia hii bali tutumie njia za kawaida za kufanya marekebisho ya Sheria zilizotungwa na Bunge. Hakuna Sheria iliyotungwa na Bunge ambayo haiwezi kufanyiwa marekebisho. Kinachotakiwa ni kupeleka mapendekezo ya vifungu au vipengele vya Sheria husika vinavyotakiwa kurekebishwa. Bunge litavijadili na kama hoja zinatosheleza vitafanyiwa marekebisho. Mimi nilipendelea busara na hekima hiyo.
Niliwaeleza wadau sababu za kuamua kutia sahihihi Sheria na kuwasihi wakubali tufanye lililo bora zaidi ambalo ni kupeleka Bungeni mapendekezo ya sheria hiyo katika maeneo ambayo tunataka marekebisho hayo yafanywe.
Nilitahadharisha kuwa hata kufanya hivyo kunaweza kuwa na ugumu wake hasa pale dhana zisizokuwa sahihi zitakapopandikizwa kwa Wabunge.
Niliwaomba tushirikiane kuhakikisha dhana potofu hazijitokezi na zinapojitokeza tuzisahihishe.
Niliwahakikishia utayari wa Serikali kushirikiana nao katika hatua zote, tangu kutayarisha mpaka kuwasilisha mapendekezo hayo Bungeni iwapo watapenda Serikali ifanye hivyo. Aidha, niliwaambia kuwa hata sisi Serikalini tulikuwa na dhamira ya kupeleka marekebisho kwa baadhi ya vifungu vya Sheria hiyo kwa sababu mbalimbali.
Nafurahi kwamba, kwa pamoja licha ya tofauti zetu kuhusu uamuzi wangu wa kutia saini Muswada tulikubaliana kushirikiana kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria hiyo, ambayo tuliyawasilisha katika Bunge lililopita.
Nafurahi na kufarijika kwamba, baada ya mjadala mkali, na Wabunge kufanya marekebisho kadhaa na hata kuingiza mambo mengine mapya, Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulipitishwa na Bunge tarehe 10 Februari, 2012. Baadaye uliwasilishwa kwangu na nikatia sahihi kuwa Sheria tarehe 20 Februari, 2012.
Sina budi pia kukitambua Chama cha Mapinduzi ambacho kilileta mapendekezo yake. Mapendekezo hayo yalizingatiwa kama ilivyofanywa kwa yale ya wadau wengine.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa vyama vya siasa vya CHADEMA, CUF, NCCR – Mageuzi na CCM na Baraza la Taifa la Asasi Zisizokuwa za Kiserikali kwa uelewa wao na ushirikiano wao kulikotuwezesha kufikia hapa tulipo katika mchakato wa kutengeneza Katiba Mpya kwa usalama, utulivu na kwa maelewano. Kwa kweli, jinsi hali ilivyokuwa huko nyuma, hatuna budi kushukuru na kujipongeza. Ni matumaini yangu na rai yangu kuwa tutaendeleza ushirikiano na utamaduni huu wa mazungumzo tuliouanzisha na kuutumia katika hatua zingine zinazofuata.
Nchi imetulia joto na jazba kuhusu Katiba havipo. Kumbe tukiamua na hasa tukizungumza inawezekana. Naomba wadau wote tuazimie kuwa mambo yaendelee hivi hata katika hatua zijazo za mchakato huu na masuala mengine muhimu kwa maslahi ya nchi yetu na watu wake.
Ndugu Wananchi;
Katika mazungumzo yetu na wadau tulikubaliana kwamba tushughulikie marekebisho ya Sheria hii kwa awamu. Kwa kuanzia tushughulikie mambo yanayohusu Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi Kuhusu Katiba ili iundwe na kuanza kazi. Baada ya hapo tuangalie mambo yahusuyo Bunge Maalum na Kura ya Maoni.
Bahati nzuri Sheria ya sasa inaelekeza kuwa Kura ya Maoni itatungiwa Sheria yake maalum, hivyo mambo yanaweza kusubiri wakati huo. Hivyo basi, baada ya muda si mrefu, Serikali na wadau tutaanza mazungumzo kuhusu mapendekezo ya marekebisho kuhusu Bunge Maalum. Kama yatakuwepo na kama kutafikiwa makubaliano, mapendekezo yatafikishwa katika Bunge letu tukufu kwa hatua zipasazo.
Ndugu Wananchi;
Bahati nzuri pia kuna kipindi kirefu kidogo wakati Tume inaendelea na kazi yake mpaka hapo Bunge Maalum litakapoanza kazi. Tume imepangiwa kukamilisha kazi yake ndani ya miezi 18 na inaweza kuongezwa miezi miwili. Wadau wanaweza kutumia sehemu ya muda huo wa Tume kushughulikia na kufanya marekebisho yahusuyo Bunge Maalum. Hata hivyo, kama mapendekezo yatakamilika mapema ni bora zaidi yafikishwe Bungeni na kushughulikiwa ipasavyo.
Wadau Kupendekeza Majina
Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa marekebisho muhimu yaliyofanywa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba katika Bunge lililopita ni kuwekwa kwa utaratibu wa wadau kupendekeza kwa Rais majina ya watu wanaoona wanafaa kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni kuhusu Katiba. Nafurahi kutoa taarifa kwamba nimekwishatoa mwaliko kwa wadau husika, yaani vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, jumuiya za kidini, asasi za kiraia pamoja na jumuiya, taasisi na makundi mengine yenye malengo yanayofanana kuleta mapendekezo hayo.
Mwaliko wangu huo umeshatangazwa katika Gazeti la Serikali Namba 66 la Ijumaa tarehe 24 Februari, 2012. Kuanzia kesho itatangazwa katika magazeti ya kawaida. Katika mwaliko huo, wadau wanatakiwa kupendekeza majina yasiyozidi matatu ya watu wanaokidhi sifa zilizotamkwa katika kifungu cha 6 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Sifa hizo ni hizi zifuatazo:-
(a) Uzoefu katika kufanya mapitio ya katiba na sifa za kitaaluma za wajumbe kwenye mambo ya katiba, sheria, utawala, uchumi, fedha na sayansi ya jamii.
(b) Jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na
(c) Umri, jinsia na uwakilishi wa makundi mbalimbali ya kijamii.
Aidha, nimeelekeza kuwa siku ya mwisho ya wadau kuwasilisha mapendekezo yao ni tarehe 16 Machi, 2012.
Wadau wanatakiwa kupitishia mapendekezo yao kwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Muungano au Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Nimewapa viongozi watendaji wakuu hao jukumu la kupokea mapendekezo ya majina na kuyawasilisha kwangu. Baada ya hapo nitashauriana na Rais wa Zanzibar kuteua Wajumbe wa Tume pamoja na Mwenyekiti na Makamu wake.
Ndugu Wananchi;
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba pia inatoa fursa kwa Rais kuteua Wajumbe wa Tume kutoka hata nje ya orodha ya wadau. Ilionekana ni vyema kufanya hivyo kwani wapo watu wengine wazuri ambao wanaweza kuwa hawamo katika makundi yaliyotajwa na Sheria hii. Aidha, upo uwezekanao kwa mapendekezo ya makundi kutozingatia baadhi ya mambo ya msingi kama vile jinsia, jiografia na mtawanyiko wa watu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kadhalika. Fursa hii aliyopewa Rais itasaidia katika kuzingatia matakwa haya ya Sheria.
Pamoja na hayo napenda kuwahakikishia kuwa iwapo nitaitumia fursa hiyo watu hao hawatakuwa wengi kuliko wale waliopendekezwa na makundi yaliyotajwa katika kifungu cha 6 (6) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu Wananchi;
Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha wadau na wananchi kwa jumla kuwa Tume ya Kuratibu na Kukusanya Maoni Kuhusu Katiba ina Wajumbe 30 tu wanaopatikana kwa idadi sawa kutoka sehemu zotu mbili za Muungano wetu yaani 15 kutoka Tanzania Bara na 15 kutoka Zanzibar. Unapoongeza Mwenyekiti na Makamu wake kwa jumla Tume itakuwa na wajumbe 32 yaani 16 kila upande. Hivyo basi, fursa ya kila aliyeleta majina kupata nafasi katika Tume si kubwa.
Nayasema haya kutahadharisha juu ya ukweli huu ili tusijipe matumaini makubwa mno na wala tusije tukashutumiana baada ya uteuzi. Hata hivyo, pamoja na ugumu wa kuchagua miongoni mwa orodha ya watu wengi wazuri, nitajitahidi tu Wajumbe wa Tume wawe watu makini, wanaowakilisha sura pana ya jamii za nchi yetu na makundi yake muhimu na utashi wa watu wa Tanzania yetu.
Tunapokwenda
Ndugu Wananchi;
Ni matarajio yangu kuwa zoezi la kuunda Tume litakamilika muda mfupi kadri inavyowezekana, baada ya kupokea mapendekezo ya makundi. Kama nilivyokwishawahi kudokeza siku za nyuma, napenda Tume ikamilike kuundwa katika robo ya pili ya mwaka huu na kuanza kazi muda mfupi baada ya hapo.
Naomba nitumie nafasi hii kutoa wito maalum kwa wananchi wenzangu kuanza kujiweka tayari kutoa maoni yao kwenye Tume. Mambo yataanza miezi michache ijayo. Najua Tume itatengeneza utaratibu wa kuelimisha wananchi kuhusu Katiba. Lakini nawaomba kila mtu binafsi yake aanze kuchukua hatua za kuifahamu Katiba iliyopo sasa ili apate ufahamu wa maudhui muhimu ya Katiba.
Kufanya hivyo kutamuwezesha kuamua kwa usahihi anataka kupendekeza nini kiwemo katika Katiba mpya. Nimeagiza Mpiga Chapa wa Serikali kuhakikisha kuwa vitabu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vinachapishwa kwa wingi ili wananchi waweze kuwa navyo na kuvisoma. Inawezekana, Timiza Wajibu Wako.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
0 Comments