KATIKATI mwaka juzi, nyota wa kike wa mipasho, Isha Mashauzi alijiengua kutoka kwa mabingwa wa mipasho hapa nchini, Jahazi Modern Taarab na mwanzoni mwa mwaka jana aliamua kuasisi kundi lake binafsi, ‘Mashauzi Classic Modern Taarab.’
Ndani ya mwaka huu mmoja tangu kuanzishwa kwake, Mashauzi Classic tayari ishahamwa na wasanii waanzilishi wasiopungua wanne, ambako kila anayeamua kuchomoka, huibua kashfa nzito, hususan kumwelekea Isha mwenyewe.
Wapo walioondoka kwa kudai kuwa wamechoshwa na ubinafsi, chuki, majungu na roho mbaya ndani ya kundi hilo, vinavyotiwa chumvi na Isha mwenyewe, huku wengine wakisema, wivu wa Isha kwa Thabit Abdul unawaweka katika wakati mgumu.
Wiki iliyopita nilibahatika kumtazama Isha alipokuwa akihojiwa na mtangazaji Hawa Hassan, kwenye marudio ya kipindi chake cha ‘Sham Sham za Pwani’ kinachorushwa kila wiki katika siku za Jumamosi, kwenye runinga ya ITV.
Hawa alimtaka Isha athibitishe shutuma nyingi hizi na zile anazotupiwa na baadhi ya wasanii wanaohama Mashauzi Classic, ambako alitoa majibu yaliyojaa hekima za hali ya juu kiasi cha kunipa msukumo wa kumtafuta ili nipate maelezo ya kina kutoka kwake.
“Unajua, yote yanayosemwa yanasemwa na watu kama mimi, wenye midomo na uhuru wa kuongea, kwahiyo inakuwa vigumu kuyazuia,” ndivyo anavyoanza kueleza Isha anayetamba sasa na kibao ‘Si Bure Una Mapungufu’, baada ya kukutana naye nyumbani kwake, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Isha anasema kuwa, mengi yanayovumishwa kila uchao juu yake yanakosa makali zaidi kutokana na yeye mwenyewe kuamua kukaa kimya bila kujibu, ambako anadai usipiomjibu mtu tayari umemwambia anyamaze.
Anasema, kinachomsikitisha zaidi na zaidi ni kuona kuwa, wote wanaomzushia kashfa na shutuma hizo ni wale chipukizi ambao.
Kwa namna hii ama ile, nguvu zake zimetumika ipasavyo kuwafikisha hapo walipo sasa.
Anazidi kusema kuwa, kwa upande wake anaona kuwa si vema kwa wasanii wanaochipukia katika muziki kujiingiza katika utamaduni wa kutafuta umaarufu kwa nguvu na badala yake wajibidiishe jukwaani kupitia vipaji walivyonavyo.
Anasema, anashangaa kuona kuwa, imekuwa ni desturi kubwa kwa wasanii wengi hapa nchini, hususan chipukizi wanapotoka kundi moja kwenda jingine, kuanzisha chuki kati yao na kundi walilohama.
"Binafsi, naona jitihada ndio silaha nzuri zaidi kwa msanii, kwasababu hata mimi nilipotoka Jahazi Modern sikuanza malumbano, ingawa wakati mwingine tulikuwa tukikosana kama ilivyo kwa wengine wote kwenye sekta mbalimbali," anasema Isha.
Anasema kuwa, jambo analopaswa kulizingatia msanii ni jinsi atakavyoweza kusimama jukwaani kuimba na kumudu kuwanyanyua vitini japo mashabiki watano, na si kutafuta umaarufu kupitia migongano isiyona msingi.
Kuhusiana na suala la kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Thabit, Isha anasema kuwa alishakataa mara nyingi na ataendelea kukataa siku zote, huku akiweka wazi kuwa uhusiano wake na Thabit unaishia kwenye muziki pekee.
Anaeleza kuwa, Thabit, kati ya wapapasa vinanda mahiri hapa nchini, ni Mkurugenzi mwenzie ndani ya Mashauzi Classic, ambako pia anamuheshimu akimwita ‘mjomba’ kutokana na kuwa ni mkubwa zaidi kwake, aliyeanza muziki kabla yake.
“Kiukweli, mtu ukishakuwa maarufu kuna mambo ambayo huwezi kuyaepuka, hivyo kwa upande wangu, nazipokea kashfa na shutuma zote ninazorushiwa na kuzichukulia kuwa ni kati ya changamoto muhimu katika maisha ya ustaa,” anasema Isha.
Hata hivyo, Isha anasema kuwa, yote yanayosemwa kwa nia mbaya kwake, yanampa ari, kasi pamoja na nguvu ya kujituma na kujibidiisha zaidi jukwaani ili kuhakikisha kuwa, malengo ya wasiopenda maendeleo yake hayatimii kirahisi.
Miongoni mwa wasanii waliohama Mashauzi Classic, ambao kwa nyakati tofauti hivi karibuni wamekuwa wakinukuliwa mara kwa mara na vyombo mbalimbali vya habari wakirusha makombora kwa Isha ni pamoja na Rahma Machupa, Zainab Machupa, Ashura Machupa na Hanifa Maulid.
0 Comments