Na Kassim Nyaki, Ndutu Ngorongoro.
Waswahili husema aungurumapo Simba mcheza nani?
Tarehe 7 Februari, 2026 Simba ameunguruma ndani ya hifadhi ya Ngorongoro eneo la Ndutu kwa uzinduzi wa Chapa mpya ya Destination Ngorongoro.
Kamishna wa Uhifadhi mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) Abdul-Razaq Badru ameongoza Menejimenti ya Mamlaka hiyo na wadau mbalimbali wa sekta ya utalii kuzindua Utambulisho Mpya wa Chapa ya 'Destination Ngorongoro” inayoashiria mwanzo mpya wa maajabu ya Ngorongoro ambayo kwa miongo mingi imekuwa ikivutia dunia kwa uzuri wake wa kipekee.
Akizindua utambulisho huo katika eneo la Ndutu Ngorongoro, Kamishna Badru ameeleza kuwa kabla Ngorongoro haijawa kivutio cha utalii kinachotambuliwa duniani, ilikuwa ni sauti yenye mwito wa uhai unaounganisha Wanyamapori, utamaduni, ardhi, historia ya mwanadamu, malikale, mazingira na maumbo mbalimbali yanayoiakisi dunia ilipojikunja na kuunda Kasoko ya Ngorongoro.
“Katika dunia ambayo ushindani wa vivutio vya utalii ni mkubwa unaozidi kuwa na Faru, tembo na visukuku pekee, Ngorongoro imeamua kujipambanua zaidi kwa mwito wenye dhamana na wajibu ndio maana tunawatambulisha rasmi muonekano mpya wa chapa ya Destination Ngorongoro kwa kufanya maboresho ya namna Ngorongoro inavyojitambulisha kwa dunia na kwa wageni kwa umahiri na muonekano ulioboreshwa” amefafamua kamishna Badru.
Moja ya maajabu ya kipekee ya asili duniani ni tukio la kuzaliana kwa nyumbu eneo la Ndutu ambapo kila baada ya saa moja takribani ndama 80,000 huzaliwa.
Katika Bonde la Olduvai na Laetoli, historia na nyayo za kwanza za binadamu zilipatikana zikitukumbusha kuwa Ngorongoro si hadithi ya wanyamapori pekee, bali ni Chimbuko la binadamu, hii ni ishara kuwa Ngorongoro ni maajabu yanayopaswa kusimuliwa hatua kwa hatua na Ngorongoro sio tu unatazamwa bali inabaki na kuishi mioyoni mwa watu.
Kamishna Badru amebainisha kuwa maboresho ya chapa ya Ngorongoro hayapo kwenye muonekano pekee bali pia yanasimuliwa kwa hadithi za Ngorongoro ili wageni wa mataifa mbalimbali wanapogika Ngorongoro kuielewa kwa undani zaidi.
Simulizi za maajabu ya Ngorongoro zinaenda sambamba na kuimarisha nyenzo kidijitali kwa uwazi zaidi na upeo wa kimataifa ambapo Ngorongoro inazungumza kupitia hadithi moja iliyounganisha mazingira hai historia ya binadamu, utamaduni, na asili na kuzungumza kwa sauti moja, mtindo mmoja, na utambulisho mmoja.
Badru anabainisha kuwa mwaka 2026 utakuwa Mwaka wa Maajabu,
chini ya kauli mbiu isemayo “Wonders Are Calling” ambayo itatekelezwa kwa awamu ikifichua maajabu ya Ngorongoro kwa kila msimu utaangazia ajabu tofauti.
Jee Maajabu hayo yatayofichuliwa kwa awamu yatakuwa ni yapii? Fuatana nasi katika taarifa zetu zijazo.
Enzi mpya ya Maajabu imeanza.
Mwito umetolewa.
Destination Ngorongoro, Experience the Wonders.




0 Comments