MEYA KIBAHA ATOA SIKU 14 KIWANDA CHA A-ONE KUACHA KUTIRIRISHA MAJI TAKA KWA WANANCHI


Mstahiki Meya Manispaa ya Kibaha Dkt Nicas Mawazo amekielekeza kiwanda cha A-One kilichopo Kata ya Visiga kuacha kutirirsha majitaka kwenye maeneo ya makazi ya watu ambapo yanaenda kusababisha athari za kiafya kwa binadamu na viumbe hai na kuwapatia siku 14 kujenga mfumo wa uchakataji maji taka.

Kiwanda hicho kinajishughulisha na ununuaji wa chupa za plastiki na kuzichakata kisha Kupata malighafi mpya, ambapo Malighafi hiyo inaweza kutumika kutengeneza bidhaa nyingine za plastiki au kuuzwa kwa viwanda vinavyohitaji malighafi hiyo. 

Mstahiki Meya Dkt Nicas ametoa maelekezo kwa kiwanda hicho kuwa hawaruhusiwi kutiririsha maji taka bila kibali kutoka kwa Bonde la Wami Ruvu na hata baada ya kupatiwa kibali ni lazima maji hayo yawe yametibiwa ili yasiwe na athari kwa wananchi wa maeneo ya karibu.


Dkt Nicas amesema, Manispaa ya Kibaha ipo makini katika kuhakikisha afya za wananchi wake zinakuwa salama, kutiririsha maji haya kwenye mazingira ya wakazi sio salama na hivyo anawapatia siku 14 kuweza kujenga mfumo sahihi wa kuchakata maji taka na wafuatilie kibali ili waruhusiwe kutiririsha maji ambayo tayari washayatibu na hayatakuwa na madhara kwa wananchi.

Afisa Mazingira Manispaa ya Kibaha, Byson Mpogoza amesema kiwanda cha A-One wamekuwa wanawapa maelekezo zaidi ya mara mbili ila wamekuwa ni watu wasiofuata maelekezo hayo na Mstahiki Meya ameagiza kiwanda hiki waandikiwe ilani na pia amewapatia wiki mbili za kurekebisha makosa yao kabla ua kuwachukulia hatua zinazostahiki.

Mstahiki Meya Dkt Nicas ameendelea na ziara zake za kukagua viwanda ndani ya Manispaa ya Kibaha ambavyo amepokea malalamiko kutoka kwa wananchi katika maeneo hayo.

Post a Comment

0 Comments