KAMANDA MPINGA ATOA ONYO KALI KWA MITANDAO INAYOPOTOSHA HABARI


KAMANDA wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mohamed Mpinga  pichani juu ametoa onyo kali kwa wamiliki wa mitandao ya kijamii kuacha kusambaza taarifa ambazo hazijafanyiwa uchunguzi na kuthibitika kama zina ukweli ndani yake.

Kamanda Mpinga, alisema hayo jijini Dar es Salaam leo wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la baadhi ya mitando kusambaza taarifa kuwa kulikuwa na ajali iliyohusisha basi la Kampuni ya Dar Express .

Alisema, onyo hilo linatokana na kitendo cha baadhi ya mitandao hiyo, juzi kusambaza taarifa kuwa kulitokea ajali iliyohusisha gari namba T 640 AXL, huku ikishindwa kutoa ufafanuzi ilikotokea jambo ambalo limezua taharuki kwa abiria wanaotumia mabasi ya Kampuni hiyo.

Mitandao iliyohusika katika kusambaza picha za ajali hiyo ya uzushi ni Bongo Mzuka, Whatsapp, Facebook na Jamii Forum.

“Baada ya picha ya basi hilo kusambazwa katika mitandao hii nilipigiwa simu na baadhi ya watu wakitaka kujua kama ni kweli kulikuwa na ajali kama hiyo, ili waweze kujua maajaliwa ya ndugu zao walio kuwa safarini wakitumia mabasi ya Kampuni hiyo,”alisema Mpinga.

Mpinga, aliwatoa hofu wananchi kuwa hakuna ajali yeyote iliyotokea ambayo ilihusisha basi la Kampuni hiyo katika siku za hivi karibuni na kwamba gari lililooneshwa katika mitandao ni la uongo kwa vile haliko barabarani.

“Niwashauri wamiliki hawa kuwa wajaribu kuwa makini na waitumie mitandao kwa ajili ya manufaa yao na watu wengune lakini si kwa matumizi kama haya ambayo yanaweza kuwaletea wengine madhara katika maisha yao na ileweke watu wa aina hiyo wakipatikana watafikishwa katika vyombo vya sheria,”alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Yudika Mremi alipotafutwa ili kutoa ufafanuzi wa ajali hiyo, alisema hata yeye alishtushwa na taarifa hizo, kwa vile gari lililooneshwa katika mitandao hiyo lilipata ajali miaka mitano iliyopita pia haliko tena barabarani tangu kipindi hicho.
Alisema baada ya kuona picha hizo alichofanya alikwenda Kituo cha Polisi Kinondoni, kufungua jalada kwa ajili ya polisi kufanya uchunguzi ambao utasaidia kujua nia ya watu waliotoa taarifa hiyo ya uongo.

Post a Comment

0 Comments