Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu wahamiaji haramu waliorejea kwao baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa Juni 29, mwaka huu katika ziara yake ya mkoa wa Kagera.
Kamishina
Mkuu wa Uhamiaji Bw.Magnus Ulungi (kulia mbele) na Afisa Uhamiaji
Mrakibu Bi.Rosemary Mkandala wakiwa katika mkutano wa Waziri wa Mambo ya
Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi alipozungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu wahamiaji haramu waliorejea kwao baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa Juni 29, mwaka huu katika ziara yake ya mkoa wa Kagera. Picha na Lorietha Laurence –Maelezo
********************************************************
NA MAGRETH KINABO – MAELEZO
SERIKALI
imesema kwamba operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu katika Kanda ya
Ziwa itaanza kwa ghafla, huku ikiendelea kusisitiza kwamba watu
wanoaishi nchini bila taratibu za kisheria kuondoka kwa hiari na mali
zao.
Kauli
hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel
Nchimbi wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu wahamiaji
haramu waliorejea kwao baada ya agizo la Rais Jakaya Kiwete alilolitoa
Juni 29, mwaka huu katika ziara yake ya mkoa wa Kagera.
“Nimeshapewa
maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kuwaondoa wahamiaji haramu
nitakapoona inafaa. Operesheni itaanza ghafla haiko mbali. Muda mwuafaka
wa kutekeleza vyombo vya dola vitasema.
“Tunatoa
wito waondoke wenyewe na mali zao bila kunyang’nywa. Wenye mali nyingi
wanatakiwa kutoa taarifa katika vituo vya polisi ili waweze
kusindikizwa. Hatutawavumilia wahamiaji haramu,” alisema Waziri Nchimbi.
Aliongeza
kuwa wahamiaji hao wanaotaka kuishi nchini wanatakiwa kurudi nchini
kwao kwanza na kufuata taratibu za kisheria kama ambavyo nchi nyingine
zinavyofanya mtu akitaka kuishi nchi yoyote anatakiwa kufuata taratibu
hizo.
Waziri
alitoa onyo kwa viongozi wa vijiji wanaoshirikiana na wahamiaji hao
kuwatunza na kusema jambo hilo ni makosa kisheria , hivyo watakaobainika
watachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumzia
kuhusu takwimu za wahamiaji hao waliorejea nchini kwao mpaka sasa ni
10,672 kati ya hao Wanyarwanda ni 6,088, Warundi 4000 na Waganda
269 ambao wametoka mkoa wa Kagera. Kwa wa mkoa wa Kigoma ni Warundi
142, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nane na katika mkoa wa Geita
Wanyarwanda 126 na Warundi 39.
Hata
hivyo Waziri Nchimbi alisema kuna wahamiaji 14 wamerejea nchini tena
baada ya kurudi makwao na kuwataka wasilione jambo hilo kuwa ni mzaha.
Aidha
Waziri Nchimbi alisema Serikali ya Tanzania inashukuru ushirikiano
unaotolewa na nchi wanazotoka wahamiaji hao kwa kuwapokea vizuri.
Alifafanua
kuwa suala la kuwarudisha wahamiaji hao si la mara ya kwanza,
lilishawahi kutokea. Huku akisisitiza kwamba tatizo linatokana na sababu
mipaka yetu mikubwa na kuna watu wasio wazalendo ambao wanawapokea na
kuwakaribisha kwa kupatiwa zawadi. Hivyo Serikali inalifanyia kazi
jambo hilo.
0 Comments