Mgeni rasimi Mama Tunu Pinda akikata utepe kuashiria uzinduzi wa huduma ya kumsadia mtoto wa kike (kushoto) kwake ni mkururugenzi Mtendaji wa Tmarc, Bibi Diana Kisaka, ambao
ni waandaaji wa mradi huo (kulia) kwa mama Pinda ni Ludovicka Tarimo,
mshauri wa masuala ya jinsia kutoka USAID anayefuatia ni Mkuu wa Vodacom
Foundation, Yessaya Mwakifulefule. Sherehe hizo zimefanyika mkoani Mtwara jana. Picha na Chris Mfinanga
Meneja wa Vodacom Foundation, Mwakifurefure, akiwahutubia wageni waalikwa.
Mama
Tunu Pinda, akishiriki na kufurahia kucheza ngoma ya asili maarufu ya
kimakonde ambayo ilikuwa ikiburusha wageni katika uzinduzi wa mradi
wakumsaidia mtoto wa kike.
**********************************************************
MKE
WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewataka Watanzania washirikiane na
wazazi na walimu kuhakikisha watoto wa kike wanasoma kwa bidii na
kutimiza ndoto zao za ukubwani.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Agosti 20, 2013) wakati akizindua Mradi
wa Hakuna Wasichoweza katika Shule ya Msingi Chilongola, iliyoko
Manispaa ya Mtwara Mikindani, mkoani Mtwara. Mradi huo unafadhiliwa na
Taasisi ya T-MARC inayojihusisha na Masuala ya Afya na Maendeleo,
umelenga kuwafikia wasichana 10,513 katika wilaya mbili za mkoa wa
Mtwara, yaani Manispaa ya Mtwara Mikindani na Wilaya ya Mtwara Vijijini.
Kabla
ya kuzindua mradi huo, Mama Pinda aliwaita wasichana watatu na kupanda
nao jukwaani na kuwahoji mmoja baada ya mwingine kwamba wangependa
kufanya nini wakiwa wakubwa.
Mwanafunzi
wa kwanza, Rahma Jamaldini (14) anayesoma darasa la saba katika shule
ya msingi Chikongola alijibu kwamba yeye angependa kuwa rubani na
akaambiwa na Mama Pinda ajitahidi katika masomo ya sayansi na hisabati
ili asome hadi Chuo Kikuu kuweza kutimiza ndoto yake hiyo.
Wa
pili alikuwa ni Eliza Paulo (8) mwanafunzi wa darasa la pili katika
shule ya msingi Chikongola aliyesema angependa kuwa mama. Aliwavunja
mbavu watu waliohudhuria uzinduzi huo alipoulizwa tena ni kitu gani
angependa kufanya mbali ya kuwa mama kwa kujibu kwamba angependa kupika.
Alipoulizwa mara ya tatu kitu kingine ambacho angependa kufanya,
akajibu kuosha vyombo. Mama Pinda allimhimiza asome kwa bidii ili awe
mama mzuri.
Wa
tatu alikuwa ni Bora Hamisi (8) ambaye pia ni mlemavu wa ngozi. Bora
anasoma darasa la pili katika shule ya msingi Msufini mjini Mtwara. Yeye
alisema angependa fundi wa kushona nguo. Naye aliambiwa asome kwa bidii
hasa somo la stadi za kazi.
Mama
Pinda alisema amewaita watoto hao ili wawe mfano wa kudhihirisha ndoto
na matamanio ambayo watoto wa kike wanayo na kwamba wasiposaidiwa kwa
kuwekewa mazingira mazuri yatakayowafanya wahitimu masomo yao, kamwe
hawataweza kutimiza ndoto zao.
“Watawezaje
kutimiza ndoto zao kama hawahudhurii masomo kama wanafunzi wengine?
Wanapaswa wasome vizuri, waende sekondari na hata vyuo vya elimu ya juu.
Tuweke miundombinu itakayowasaidia kuhudhuria masomo bila kukosa,”
alisema.
Mapema, Mkurugenzi
Mtendaji wa TMARC, Bi. Diana Kisaka alisema mradi huo umelenga kuinua
uelewa wa wasichana kuhusu miili yao na mabadiliko yanayotokea katika
kipindi cha balehe; kuwapa ufahamu kuhusu makundi mbalimbali miongoni
mwa jamii iliyowazunguka na kuwapa upeo wao kuhusu umuhimu wa kuzingatia
malengo yao katika maisha.
Naye
Mkuu wa Vodacom Foundation, Bw. Yesaya Mwakifulefule alisema Vodacom
Foundation imechangia sh. milioni 160 kwenye Mradi wa Hakuna Wasichoweza
kwani inatambua umuhimu wa elimu na suala zima la kuendeleza wasichana
kielimu.
“Vodacom
Foundation inashugulika na masuala ya elimu kwa kuchangia madawati na
teknolojia ya habari na mawasiliano katika shule mbalimbali hapa nchini.
Hapa Mtwara tumetoa kompyuta 20 kwenye shule ya sekondari ya wasichana
ya Mtwara ambazo zimeunganishwa na intaneti ya Vodacom,” alisema.
Naye mwakilishi kutoka Shirika la Misaada la Maendeleo la Marekani (USAID), Bi.
Ludovicka Tarimo, alisema taasisi yake imechangia Dola za Marekani
196,650 kwenye mradi huo ambao wanaamini kupitia utekelezaji wake,
utawasaidia mamilioni ya watoto wa kike hapa nchini kupata mafunzo ya
kujitambua na hatimaye kufanikiwa kielimu.
0 Comments