RAIS MAGUFULI MGENI RASMI MAADHIMISHO YA MIAKA 50 BOT

JUNI 22, 2016 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha sherehe za kuadhimisha miaka 50 tangu Benki Kuu ya Tanzania ilipoanzishwa.

Sherehe hizi zitafanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam tarehe 22/06/2016 ambapo mgeni rasmi atazindua vitabu viwili na kufuatiwa na kongamano litakaloshirikisha wataalam mbalimbali wa uchumi wakiwemo magavana 20 wa benki kuu kutoka nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika. Mada kuu katika Kongamano hilo itakuwa:

“Beyond Aid and Concessional Borrowing: New Ways of Financing Development in Africa and its Implications”, (yaani namna ya kupata fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya misaada na mikopo nafuu na athari zake) itakayowasilishwa na Prof. Justin Lin wa Chuo Kikuu cha Peiking, China.

Mada hii imechaguliwa kwa kuzingatia changamoto ambazo serikali za Afrika zinakumbana nazo katika kugharamia miradi ya maendeleo wakati ambapo misaada na mikopo nafuu imekuwa ikipungua kwa kiasi kikubwa.

Wachumi waliobobea wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo magavana 20 kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika mashariki (EAC) na wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) watashiriki katika kongamano hilo. Vitabu vitakavyozinduliwa siku hiyo ni (i) “Tanzania: The Path to Prosperity”

kinachoelezea masuala yanayohusu sera za uchumi nchini Tanzania ambacho kimeandikwa na wachumi waliobobea wa ndani na nje ya nchi, na kimechapishwa na Oxford University Press. (ii) Kitabu cha pili ni cha miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania kiitwacho “50th Anniversary of the Bank of Tanzania:

Evolution of the Bank of Tanzania’s Role and Functions”, ambacho kinaelezea historia, majukumu, mafanikio na changamoto za Benki Kuu katika kipindi cha miaka 50 na matarajio ya Taasisi hii ya Umma katika maendeleo ya taifa katika kipindi cha miaka 50 ijayo.

Aidha, Tarehe 11/6/16 Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa atakuwa Mgeni Rasmi kwenye matembezi ya hisani ya wafanyakazi wa Benki Kuu kutoka makao makuu ya Benki hadi viwanja vya Mnazi Mmoja kuchangia ununuzi wa madawati ya shule za msingi kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Benki.

Wafanyakazi wa Benki Kuu walioko matawini Mtwara, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya, Zanzibar na Chuo cha Benki Mwanza nao pia watafanya matembezi ya hisani kwenye mikoa yao.

Pamoja na matembezi kutakuwa na maonesho yaliyoandaliwa na Benki Kuu katika viwanja vya Mnazi Mmoja yenye lengo la kuwapa wananchi historia ya taasisi hii, ilikotoka, ilipo na inakoelekea katika kutekeleza majukumu yake.

Benki Kuu ingependa kuwakaribisha wananchi kufika kwa wingi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja siku hiyo ya tarehe 11/6/16 kujifunza mengi kuhusu taasisi hii ya umma. Aidha, tunawaomba wananchi kufuatilia vipindi mbalimbali vya redio na makala kwenye magazeti ambapo mengi kuhusu historia, changamoto, mafanikio na matarajio ya Benki yataelezwa na viongozi mbalimbali wa Benki wa sasa na waliopita.

Benki Kuu ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 1965 na kuanza kutoa huduma rasmi tarehe 14 mwezi Juni mwaka 1966. Katika kipindi cha uhai wake, Benki Kuu ya Tanzania imetimiza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kulingana na mahitaji ya taifa yalivyojitokeza mwaka hadi mwaka.

Imetolewa na: Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki

Post a Comment

0 Comments