CHAMA cha Wasambazaji wa Filamu nchini kimefungua shauri Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC), ya kupinga mpango wa kushushwa kwa bei ya filamu za Kibongo kutoka sh. 3,500 ya sasa hadi sh. 1,000 kwa madai kitendo hicho kinaweza kuua soko na kusababisha washindwe kujiendesha kama ilivyo sasa.
Mwenyekiti wa chama hicho, Emmanuel Myamba ‘Pastor Myamba’, alisema
wamelazimika kufungua kesi baada ya kuona juhudi zao za kukaa meza moja na
wasambazaji wenzao Kampuni ya Steps Entertainment ambao ndio wana nia ya
kushusha bei hiyo kushindwa kufikia muafaka.
“Tumekuwa na vikao vya mara kwa mara na viongozi
wa Steps juu ya suala hili la kutoshusha bei ya filamu, lakini wamekuwa wagumu
wa kuelewa, hivyo tumeona dawa pekee ni kufungua shauri la kesi FCC, ambao
tunaamini wao watatusaidia juu ya jambo hili ambalo linatuumiza vichwa vyetu,”
alisema Pastor Myamba.
Tangu mpango huo wa kushushwa kwa bei ya filamu
kutangazwa na Steps, kumekuwa na mgawanyiko kwa wasanii, wasambazaji na
watayarishaji wa sinema hizo, huku wengine wakipongeza hatua hiyo kwamba
itaongeza mauzo ya kazi zao, kwani watakuwa wanapambana na maharamia ambao kwa
sasa wanauza CD kwa sh. 700 hadi 1,000.
Baadhi ya watayarishaji wanaopeleka kazi zao
Steps, wanadai kumshauri msambazaji huyo kufanya hivyo ili kupambana na
maharamia, lengo la pili ni kuwafikia watazamaji wengi, jambo ambalo linapingwa
vikali na wasambazaji wazawa.
0 Comments