Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amesema mkoa upo salama pamoja na uwepo wa changamoto ya idadi kubwa ya wahamiaji haramu kutoka nchi zinazopakana na mkoa, wanaolenga kuingia nchini kujitafutia kipato sambamba na ukosefu wa hali ya amani na utulivu maeneo wanayotoka.
Sirro ametoa kauli hiyo alipokutana na Kamishna wa Polisi Jamii CP. Faustine Shilogile akiwa mkoani Kigoma kwa ajili ya kuendesha mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa wa Polisi Jamii Kanda Namba tano inayohusisha mikoa ya Kigoma, Kagera na Tabora.
Balozi Sirro ameuomba uongozi wa Serikali kupitia jeshi hilo kuendelea kuongeza watendaji katika mkoa, kutokana na uhitaji mkubwa uliopo.
Kwa Upande wake Kamishna Shilogile amesema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kuboresha utendaji kazi wa Jeshi hilo ikiwemo kuongeza kwa kiasi kikubwa nyenzo sa usafiri ili kurahisisha ufikiwaji wananchi na kutatua changamoto zao za kiusalama.

0 Comments