KIBA AWA KIVUTIO TAMASHA LA SAUTI ZA BUSARA ZANZIBAR , AWAACHA KWENYE MATAA WAANDISHI WA HABARI


MWANAMUZIKI wa kizazi kipya Ally Kiba aliwaacha kwenye mataa waandishi wa habari kutoka katika vyombo mbalimbali duniani ambao walikuwa wakisubiri kufanya mahojiano naye kwa kisingizio kwamba amechoka.
Waandishi hao ambao walikusanyika kwenye ukumbi wa wanahabari uliopo kwenye jengo la Ngome Kongwe  katika tamasha la Sauti za Busara ambalo lilifanyika  visiwani Zanzibar.
Huo ndiyo ulikuwa utaratibu ulioweka kwamba  pindi msanii anapomaliza kufanya shoo hupandishwa ghorofani ambako kuna chumba cha waandishi wa habari hivyo huanza kufanya mahojiano kwa lugha ya Kiingereza ili kutoa fursa kwa vyombo vya habari vya nje kuweza kuzungumza na msanii husika.
Aidha licha ya  kukwepa mkufanya mahojiano  na waandishi lakini msanii huyo  kiba aliweza kuonesha kupevuka kisanii kutokana na kuimba  muziki wake ‘Live’ na kukonga nyoyo za mashabiki waliofurika Ngome Kongwe katika ambako tamasha hilo la muziki lilifanyika kati kati ya Februaru 12 hadi 15 Zanzibar.
Kiba alipanda jukwaani saaa 6:05 usiku huku akianza na wimbo wake wa Kimasomaso ambapo katikati ya wimbo huo aliweza kuchomekea  beti kadhaa ambazo ziliimbwa   na marehemu Issa Matona katika wimbo wake wa ‘Kimasomaso ambao mara nyingi huchezwa maharusini na kujipatia umaarufu.
Baada ya wimbo huo Kiba aliendelea kuweka bandika bandua kwa kuimba nyimbo zake kama vile ‘Single Boy’,  uliofuatiwa na wimbo wa  ‘Hadithi’,  ‘Mapenzi yanaRun Dunia’, ulifuatiwa na ‘Dushelele’  , ‘Asubuhi’ na nyinginezo.
Ilipofika saa 6:48 Kiba alimpandisha mdogo wake Abdul Kiba ambapo wakaimba pamoja  na kucheza pamoja jambo ambalo lilizidi kuamsha ari   ya muziki kwa mashabiki , wakaonyesha shoo ya aina yake ndugu hao wawili na kushangiliwa.
Aidha ujio wa Kiba katika tamasha hili umeonesha kukubalika kwake na muziki wa Bongo Fleva huku akifanikiwa  kuacha gumzo na kiu kwa mashabiki hata pale alipomaliza kazi yake jukwaani ambako alidumu kwa kuda wa saa moja na robo.
Kiba alipanda jukwaani kwenye shoo ya tamasha hilo katika siku ya kwanza na kufanikiwa kukonga nyoyo za mashabiki wake.
Wasanii wengine ambao walitoa burudani ni pamoja na Mwahiyerani (Tanzania), Aline Frazao (Angola), Liza Kamikazi ((Rwanda),Zee Town Sojaz  (Zanzibar), Mpamanga (Madagascar), Rico Single &Swahili Vibes (Zanzibar), Ihhlashi Elimhlope (Afrika Kusini) na  Sarabi (Kenya).
Wengine  ni DCMA Young Stars (Zanzibar), Bonaya Doti (Kenya), Culture  Musical Club (Zanzibar), Tanganyika (Msafiri  Zawose), Eric  Aliana ( Cameroon),Maramaso (Kenya) na Isabella  Novella (Msumbiji).
Tamasha hili  la Sauti za Busara  linafanyika  kwa mara ya 12 limeanza Februari 12 na litafikia tamati Februari 15.

Post a Comment

0 Comments