ALLY KIBA AAHIDI MAKUBWA SAUTI ZA BUSARA

Kutoka  kushoto ni Khadija Kalili, msanii Ally Kiba na Mwanamkasi Mhando mara baada ya kufanyika kwa mkutano wa Sauti za Busara katika hoteli ya Holiday Inn, Jijini Dar es Salaam jana.
 
MSANII nyota nchini wa muziki wa kizazi kipya, Ali Kiba, ameahidi kuonyesha kipaji na uwezo wake wa hali ya juu alio nao katika muziki kwenye tamasha la Sauti za Busara litakalofanyika Mji Mkongwe, Zanzibar, Februari 12-15, mwaka huu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kiba alisema atahakikisha anawafunika wasanii wengine kutoka mataifa mbalimbali ili hata wakiondoka, waondoke na sifa kwamba Tanzania kuna wasanii wenye sifa zote.

Naye Mwenyekiti wa Busara Promotion, Simai Mohammed, alisema tamasha la Sauti za Busara huwakutanisha wasanii na watu kutoka kila pembe ya dunia na kusherehekea pamoja muziki wa Afrika katika ardhi ya Zanzibar.

Alisema makundi 37 yamechaguliwa kushiriki Tamasha la Sauti za Busara mwaka huu, ambapo kati ya hayo, 19 yatakuwa ya hapa nchini na idadi iliyobaki ikiwa ni kutoka mataifa ya nje.

Wasanii ama kundi waliloalikwa mbali ya Ali Kiba ni pamoja na Leo Mkanyia, Mohammed Ilyas, Msafiri Zawose, Kundi la Mgodro, Bendi ya Ifa, Mabantu Afrika na wengineo.

Kwa upande wa wasanii wa kimataifa ni pamoja na mwana hip hop, Blittz the Ambassador (Ghana), anayeishi Brooklyn, Ihhashi Elimhlophe, Brother Moves On (Afrika Kusini) na Octopizzo (Kenya).

Wengine ni Sarabi (Kenya), Aline Frazao (Angola), Tcheka (Cape Verde), Isabel Novella (Msumbiji), Thais Diarraft Noumouconda (Senegal), Tsiliva (Madagascar), Djimawi Afrika (Algeria) na wengineo.

Mbali ya maonyesho ya muziki, pia tamasha litaonyesha filamu za muziki zikiwamo ‘The Last Song Before The War (Mali), Maramaso (Kenya), 100% Dacar (Senegal), pia watamuenzi marehemu Bi. Kidude kwa kuonyesha filamu ya muziki ya ‘I Shot Bi Kidude’ iliyoongozwa na Andy Jones kutoka Uingereza.

Tamasha hilo linafanyika kwa mara ya 12 sasa huku likiwa na kauli mbiu isemayo: ‘Amani Ndio Mpango Mzima’.

Post a Comment

0 Comments