Vumbi awataka Choki, Asha Baraka kumaliza tofauti zao



Ally Choki

Asha Baraka

Alain Dekula Kahanga 'Vumbi'
MWANAMUZIKI wa zamani wa bendi ya Marquiz Original, Alain Dekula 'Vumbi' anayefanya shughuli zake za muziki nchini Sweden, amewasihi wakurugenzi wa bendi za Extra Bongo, Ally Choki na mwenzake wa African Stars 'Twanga Pepeta' Asha Baraka kumaliza tofauti zao.
Vumbi alisema amekuwa akifuatiliwa malumbano baina ya wakurugenzi hao kupitia mitandao ya kijamii na kushangazwa kusikia wawili hao wakiapiana kutozikana wala kuhudhuria mazishi ya mwenzake akidai hadhani ni jambo zuri au lenye tija kwa muziki wa Tanzania.
Mcharaza gitaa la solo huyo, alisema ni vyema wawili hao wakaa chini na kumaliza tofauti zao kwa masilahi ya muziki wa Tanzania ambao alidai bado una kazi pevu kuweza kujitangaza nje ya mipaka ya Tanzania kama alivyoutangaza marehemu Dk Remmy na kundi la Tatu Nane.
"Sifurahishwi na uhasama unaoendelea baina ya Asha Baraka na Ally Choki, ningependa wakae chini na kuzika tofauti zao kwa masilahi ya muziki wa Tanzania, malumbano kati ya makundi siyo jambo jipya, lakini haikuwahi kufikia watu kukataliana kuzikana," alisema Vumbi.
Vumbi alisema anafahamu 'bifu' za kisanii hufanywa kokote duniani kwa lengo la kuongeza soko na kuvuna mashabiki, lakini siyo kama uhasama uliopo baina ya watu hao wawili ambao ni moja ya mihimili mikubwa ya muziki wa dansi Tanzania kwa kusaidia ajira ya watu wengi.
"Naomba unifikishie salamu zangu wakae chini na kusameheana kama kuna tatizo baina yao, ili kusaidia dansi lizidi kusonga mbele, malumbano na 'bifu' zitumike kuinua soko la muziki na sio  kuwekeana kinyongo kama ninachosikia na kukisoma mitandaoni," alisema.
Kauli ya Vumbi imekuja baada ya wakurugenzi hao kunukuliwa wakiapiana kwamba 'hawapendani' na katu mmoja wao asihudhurie wala kumzika mwenzake akitangulia kufa kutokana na kutofautiana mara baada ya kuachana kufanya kazi sehemu moja.
Choki alikuwa mmoja wa wanamuziki wa Twanga Pepeta akiingia na kutoka kabla ya kuanzisha Extra Bongo ambayo imekuwa ikiwanyakua wanamuziki toka kwa wapinzani wao hao, huku yeye akifikishwa mahakamani akidai gari analodai alipewa kwa makubaliano.

Post a Comment

0 Comments