PAMBANO LA YANGA, MTIBWA SUGAR LAINGIZA MIL 125/-



 
Mechi namba 100 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 2 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 limeingiza sh. 125,181,000.
Watazamaji 22,030 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo iliyochezwa kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 30,356,002.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 19,095,406.78.
Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo 19,583 walikata tiketi hizo na kuingiza sh. 97,915,000.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 15,435,255.48, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 9,261,153.29, Kamati ya Ligi sh. 9,261,153.29, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 4,630,576.64 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 3,601,559.61.
WANYARWANDA KUCHEZESHA MECHI YA STARS, CAMEROON
Waamuzi kutoka Rwanda wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ndiyo watakaochezesha pambano katika Tanzania na Cameroon litakalochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi wa katikati atakuwa Munyemana Hudu wakati wasaidizi wake ni Simba Honore na Ndagizimana Theogine wakati mwamuzi wa mezani ambaye pia anatambuliwa na FIFA atakuwa Oden Mbaga wa Tanzania.
Hudu na wenzake watawasili nchini kesho (Februari 4 mwaka huu) saa 12.40 jioni kwa ndege ya RwandAir na wamepangiwa kufikia kwenye hoteli ya JB Belmont. Mechi ambayo ni moja kati ya nyingi zitakazochezwa siku hiyo (FIFA Date) itafanyika kuanzia saa 11 kamili jioni.
KUNDI LA AKINA ETO’O KUTUA KESHO DAR
Wakati kundi la kwanza la timu ya Cameroon lenye watu 13 linaingia nchini leo (Februari 3 mwaka huu) saa 4.40 usiku, kundi la pili linaloongozwa na nahodha wa timu hiyo Samuel Eto’o linatua kesho (Februari 4 mwaka huu) saa 3.45 asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Eto’o anayechezea timu ya Anzhi Makhachkala ya Urusi atatua kwa ndege ya Kenya Airways akiwa na Herve Tchami wa Budapest Honved ya Hungary, beki Nicolas Nkoulou wa Marseille ya Ufaransa, mshambualiji Jean Paul Yontcha wa SC Olhanense ya Ureno na daktari wa timu Dk. Boubakary Sidik.
Saa moja baadaye baada ya Eto’oo kutua na wenzake, Kocha wa timu hiyo Jean Paul Akono na msaidizi wake Martin Ndtoungou watawasili saa 4.40 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways wakitokea Afrika Kusini.
Kesho pia kuna kundi lingine litakaloingia saa 4.40 usiku kwa ndege ya KLM ambalo lina beki Jean Kana Biyick wa Rennes ya Ufaransa, mshambuliaji Fabrice Olinga wa Malaga FC ya Hispania, beki Allan Nyom wa Udinese ya Italia ambaye yuko kwa mkopo Granada ya Hispania na beki wa kushoto Henri Bedimo wa Montpellier ya Ufaransa.
Wachezaji waliobaki wakiongozwa na kiungo wa Barcelona, Alexandre Song watawasili Februari 5 mwaka huu kwa muda tofauti kwa ndege za KLM na Kenya Airways.

Post a Comment

0 Comments