JOYCE KIRIA 'SUPER DUPER WOMAN'
Na HERIETH MAKWETTA
Habari hii kwa hisani ya gazeti la Mwanaspot.'UGUMU wa Maisha ni Kipimo cha Akili'. Huu ni usemi uliozoeleka katika maisha ya kijamii hasa kwenye miaka ya sasa ambapo hali ya uchumi imekuwa ikizidi kuwa ngumu.
Katika ugumu wa maisha huo kuna walioshindwa kabisa kujikwamua hadi kukata tamaa. Lakini kuna ambao wameutumia ugumu huo kutafuta namna ya kujikomboa, ndiyo wanaozungumzia kwenye usemi huu.
Mmoja wa watu hao ni mtangazaji ambaye pia ni Mmiliki wa Local Media Entertainment, kampuni inayoendesha vipindi vya televisheni vya 'Wanawake Live' na 'Bongo Movie', vinavyorushwa na Kituo cha EATV, mwanadada Joyce Kiria.
Utumwa pasipo malipo sahihi na kutokuwa na uhuru wa maamuzi, vilikuwa sehemu ya maisha yake kwa muda mrefu. Ilikuwa ni baada ya kumaliza elimu yake ya msingi.
"Unajua natoka katika familia ya hali ya chini, hivyo nilipomaliza Darasa la Saba sikuwa na namna ya kuendelea na masomo," anasema.
"Nilianza kwa kufanya kazi za ndani za u-hausigeli, nilifanya kazi hii kwa miaka miwili. Sikuifurahia sana.
"Baadaye niliona nisonge mbele, niliiacha kazi hiyo na nikajiunga katika genge la mama ntilie, nilifanya kazi hapo kwa muda mpaka nilipoamua kuanza kuchoma chapati."
Hata hivyo anasema hakudumu na kazi hiyo kwani hakuwa akipatana na moto hivyo akatafuta kazi katika kiwanda cha mablanketi, Chang'ombe jijini Dar es Salaam.
"Nikafanya kazi kwa muda pale lakini baadaye nikapata nafasi ya kazi katika duka moja Kariakoo, jijini Dar es Salaam, hapo ilikuwa tayari imefikia mwaka 2000," anaongeza.
"Niliendelea na kazi yangu na baadaye nilipata mtaji wa kuniwezesha kufungua biashara yangu."
Anasema alianza biashara zake rasmi kwa kupigisha simu katika vibanda vidogo, mtaji ulikua na baadaye alifungua duka la vifaa vya shule na mapambo, lakini baadaye akairudia biashara ya nguo.
"Baada ya kufanikiwa kukuza mtaji wangu, niliingia tena katika biashara ya nguo, na nikaanza kununua nguo za jumla kutoka Dubai, Falme za Kiarabu," anasema.
"Siku moja nikaenda na kununua nguo mwenyewe huko Falme za Kiarabu. Nilirudi na kuona nguo hizo zimejaa sana Kariakoo na bei yake ipo chini, hapo ndipo mtaji wangu ukafa au kwa maneno mengine nifilisika."
Anasema baada ya kushindwa biashara akaamua kumwona, Amina Chifupa (sasa marehemu) ambaye alikuwa mteja wake wa nguo na kumweleza shida yake.
"Amina ambaye wakati huo alikuwa anafanya kazi redio ya Clouds akanishauri nianze utangazaji kwani aliona nina kipaji, hivyo nilianza kazi hiyo pale Clouds mwaka 2006. Mwaka 2008 nikaolewa," anasema.
KUVUNJIKA KWA NDOA YA AWALI
Joyce, ambaye sasa ni mke halali wa Henry Kilewo, ndoa yake ya kwanza ilikuwa mwaka 2008 alipooana na Nelson Joshua 'DJ Nelly'.
"Muda mfupi baada ya ndoa nikaanza kuonja machungu yake, niliishi maisha ambayo sikuchagua, hii ilikuwa ni baada ya kuolewa," anasema.
"Niliamua kuachana na mume, unajua ilifikia hatua nilihisi ningeweza hata kuwekewa sumu katika chakula, yalikuwa ni maisha ya chuki.
"Hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuyajua mengi ambayo niliamua rasmi kuanza kuyafanyia kazi nikiwa kama mwanamke niliyejitolea kutetea haki za wanawake."
Anasema alianza kwa kudai talaka ambayo ilikuwa ngumu kutolewa kwani ndoa aliyofunga ilikuwa ni ya Kikristo.
"Nilifanikiwa kupewa talaka yangu na hapo ndipo ukawa mwanzo wa kuanzisha kipindi cha Wanawake Live nikiwa na dhamira ya kweli ya kutetea Haki za Wanawake.
WITO WAKE KWA JAMII
Joyce ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Kilimanjaro, anasema tatizo lililopo hapa nchini ni mfumo dume, ambao umekithiri.
"Mwanaume anasahau kutunza familia yake na kutokomea kusikojulikana, kwa sababu ya uchumi mdogo familia yake inaingia kwenye taabu, hali hii haivumiliki na ndiyo mwanzo wa kuvunjika kwa ndoa nyingi," anasema.
"Pia changamoto za kimaisha ni nyingi, wapo wanawake wenye kipato, lakini kutokana na mfumo dume wanalazimika kuacha kila kitu kikiwa chini ya waume zao ambao baadaye huwasaliti."
Anasema kupitia kazi yake ya sasa amepania kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ili iachane na na mfumo huo kuweza kutoa haki sawa kwa wote.
0 Comments