Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo iko katika mzunguko wa pili inaendelea tena leo (Machi 2 mwaka huu) na kesho (Machi 3 mwaka huu) baada ya kusimama kwa wiki moja kupisha mechi kati ya timu ya Taifa (Taifa Stars) dhidi ya Msumbiji (Mambas).
Leo kwenye Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam kutakuwa na mechi kati ya JKT Ruvu na Toto Africans. Mechi za kesho (Machi 3 mwaka huu) ni kati ya Oljoro itakayokuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
Nayo Polisi Dodoma ikiwa chini ya makocha Rashid Chama na Henry Mkanwa itakuwa ugenini kwenye mashamba ya miwa ya Mtibwa mjini Turiani kuikabili Mtibwa Sugar ya huko.
Machi 5 mwaka huu Moro United inayofundishwa na Hassan Banyai itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo iko chini ya Charles Kilinda katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mechi za Machi 7 mwaka huu ni kati ya Oljoro na Toto African (Sheikh Kaluta Amri Abeid), Simba na Kagera Sugar (Uwanja wa Taifa) wakati Azam itakuwa mwenyeji wa Coastal Union kwenye Uwanja wa Chamazi.
CHIPUKIZI AINGIA KITUO CHA VIPAJI SENEGAL
Mchezaji Sifael Orgenes Mollel (14) amechaguliwa katika mpango wa kukuza vipaji wa Aspire Football Dream ambao uko chini ya Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwenda kituo cha vipaji (centre of excellence) kilichoko Dakar, Senegal.
Mollel kutoka kituo cha Karume alichaguliwa katika mchakato wa mwaka jana uliofanywa na mng’amua vipaji vya soka (scout) kutoka Hispania kwa niaba ya Aspire Football Dreams yenye makao makuu yake Doha, Qatar.
Mpango huo wa Aspire Football Dreams kwa Tanzania una vituo 14 na mchakato wa kusaka mchezaji mmoja kila mwaka uhusisha vituo vyote hivyo ambapo kila kimoja kinatakiwa kuwa na watoto wasiopungua 176.
Mbali ya Karume, vituo vingine ni Kigamboni, Kawe, Tandika, Makongo, Ukonga, Kitunda, Mbagala, Magomeni, Morogoro, Bagamoyo mkoani Pwani na Tabata.
Mollel atakuwa kwenye kituo hicho cha Dakar kwa muda usiopungua miaka mitatu na anatarajiwa kuondoka nchini Machi 6 mwaka huu. Kwa mwaka wa kwanza wazazi wake watalipwa dola za Marekani 2,500, wa pili dola 2,750 na wa tatu dola 3,000.
Mpango wa Aspire Football Dreams ambao unafadhiliwa na mtoto wa Mfalme wa Qatar una vituo viwili vya kuendeleza watoto wenye vipaji (centre of excellence) ambayo viko Doha na Dakar.
Lakini mpango huo unaendeshwa katika nchi 16 tofauti duniani. Nchi hizo ni Cameroon, Costa Rica, Gambia, Ghana, Guatemala, Ivory Coast, Kenya, Mali, Nigeria, Paraguay, Rwanda, Senegal, Tanzania, Thailand, Uganda na Vietnam.
U17 KUJINOA KWA RUVU SHOOTING
Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) leo (Machi 2 mwaka huu) imeanza kambi yake ya wiki moja ambayo hufanyika kila mwezi jijini Dar es Salaam chini ya kocha Kim Poulsen.
Serengeti Boys inayofanya mazoezi Uwanja wa Karume itahitimisha kambi hiyo Machi 9 mwaka huu kwa kucheza mechi na timu ya U20 ya Ruvu Shooting ya mkoani Pwani ambayo iko Ligi Kuu ya Vodacom.
Baada ya Serengeti Boys kumaliza kambi Machi 9 mwaka huu, siku hiyo hiyo timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) nayo itaingia kambini chini ya Poulsen katika mpango wa timu hizo kufanya mazoezi ya wiki moja kila mwezi na kucheza mechi moja.
0 Comments