Mwanamuziki nyota wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars wana Twanga Pepeta, Ramadhani Athumani maarufu kama Dogo Rama amemruka kimanga msanii aliyenukuliwa na gazeti moja la kila wiki akimponda kuhusu uwezo wake kimuziki.
Akiongea na waandishi wa habari juzi, Dogo Rama alisema kuwa, cha kushangaza ni kuwa yeye hamjui kabisa huyo msanii anayemuandika vibaya magazetini na hata habari zake kama ni mwanamuziki au msanii wa fani zingine kama uchongaji vinyago au kibarua mbeba zege.
Akasema, hayumkini kuamini kuwa maneno yaliyoandikwa kwenye gazeti lile (akilitaja) yalinukuliwa kwa mtu anayejua sanaa. Akaongeza kuwa, tatizo kubwa ni uwezo mdogo wa kujua mambo ndiyo unawasumbua watu wengi hata kushindwa kutofautisha pumba na mchele au mbivu na mbichi huku akitoa msemo wa 'mti wenye matunda matamu ndio unaopigwa mawe'.
"Nashangaa kusikia eti kuna mtu anajiita 33, hivi ni nani? Mbona simjui? Unajua siwezi kushindana na giza, yeye ni giza totoro! Hivi ni mtu au namba? Anafanya kazi gani za sanaa? Mwanamuziki au mchonga vinyago? Isije ikawa ni tingo wa fuso au mbeba zege!? Au mpambaji wa maharusi? Manake fani ziko nyingi," akamaka Dogo Rama huku akionesha kukereka.
Hata hivyo, Dogo Rama alisema hayumbishwi na maneno ya watu au mashabiki wachache wasiomtakia mema katika ufanisi wa kazi zake kwa vile anajiamini na ana uhakika na anachokifanya ndio maana akapata kazi katika bendi bora na kongwe ya dansi la vijana ya African Stars.
Akazidi kusema, angekuwa msanii 'boya' kama walivyo wengine wanaovamia na kubabaisha katika fani zao asingeweza kupokelewa katika bendi yenye historia kubwa Tanzania katika miaka kumi na ushee ya karibuni ambayo karibu kila mwanamuziki huota kuifanyia kazi kama ilivyo kwa wanasoka wengi kuzitamani Yanga au Simba.
0 Comments