NAIBU WAZIRI  MILYA AKUTANA NA  UONGOZI  WA JUMUIYA  YA WAISLAMU  WA AHMADIYA 

Naibu Waziri Millya akutana na Uongozi wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Mhe. James Kinyasi Millya (Mb), amekutana na Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Shekh Khawaja Muzaffar Ahmad, aliyetembelea Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki jijini Dar Es Salaam kwa lengo la kujitambulisha na kuwasilisha salamu za pongezi kwa Uongozi wa Wizara kwa utekelezaji uliotukuka wa majukumu yake.

Mhe. Millya, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo (Mb), aliishukuru Jumuiya ya Ahmadiyya kwa juhudi zake katika kutoa huduma mbalimbali za kijamii na kibinadamu maeneo mbalimbali nchini. Aliendelea kueleza kuwa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania imekuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya taifa na kwamba Serikali inatambua na kuthamini mchango wa taasisi hiyo katika kuleta maendeleo endelevu nchini katika sekta mbalimbali.

Ameongeza kuwa Wizara ipo tayari kutoa ushirikiano wowote utakaohitajika ili kuwezesha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo, ikiwemo utekelezaji wa programu za kurejesha kwa jamii na mikutano, ikiwa ni pamoja na Mkutano Mkuu wa Mwaka (Jalsa Salana) unaotarajiwa kufanyika Septemba 2026, na Mkutano Mkuu wa Kimataifa wa Jumuiya ya Ahmadiya Duniani unaopangwa kufanyika mwezi July 2026 nchini Uingereza.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Abdalah Kilima pamoja na maafisa waandamizi wa Wizara.

 
Kwa upande wake, Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Shekh Khawaja Muzaffar Ahmad, amesema kuwa tangu jumuiya hiyo ilipoanzishwa mwaka 1934, imefanikiwa kuanzisha matawi 450 nchini na kueneza mafundisho ya Dini ya Kiislam kwa misingi ya Qur’an Tukufu, huku ikikuza amani, upendo, udugu, uvumilivu, heshima, na kusaidia watu wote bila kujali kabila, imani au itikadi zao.

Sheikh Ahmad ametaja miradi na programu za kurejesha kwa jamii inayotekelezwa na jumuiya hiyo kuwa ni mradi wa hospitali, shule za msingi na sekondari mkoani Morogoro, chuo cha mafunzo cha ufundishaji dini kwa wazawa, uchimbaji wa visima kuunga mkono juhudi za serikali katika kampeni yake ya Kumtua ndoo mama, ambapo hadi sasa wamechimba visima  500 katika maeneo mbalimbali nchini na mradi wa kuendeleza Kijiji cha Kisasa katika Mkoa wa Geita. 

Shekh Ahmad aliambatana na viongozi wakuu wa Jumuiya hiyo, wakiwemo Naibu Amiri-1Shekh Abid Mahmood Bhatti, Naibu Amiri-2 Shekh Abdurahman M. Ame, Katibu wa Mambo ya Ndani Bw. Yahya A. Kambaulaya, Katibu wa Mambo ya Nje Bw. Abdallah Kombo na Katibu wa Sauti na Video Shekh Asif M. Butt.


Post a Comment

0 Comments