Na Tiganya Vincent-MAELEZO-Dar es salaam
SERIKALI ya Japan imepatia Tanzania msaada wa shilingi bilioni
28.2 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu ya uboreshaji wa usafiri
jijini Dar es salaam na kilimo hapa nchini.
Msaada huo umesainiwa (leo)
jijini Dar es salaam na Balozi wa Japan hapa nchini Masaki Okada kwa
niaba ya Japan na Waziri wa Fedha Dkt. William Mgimwa kwa niaba ya
Serikali ya Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kusaini msaada huo Waziri wa Fedha Dkt .
Mgimwa alisema kuwa mradi wa kwanza utahusisha upanuzi wa barabara ya
Kilwa na ile ya Bandari ambapo jumla ya shilingi bilioni 20 zitatumika
katika kukamilisha mradi huo.
Aliongeza kuwa mradi mwingine ni ule wa ujenzi wa barabara za
juu(flyover) katika makutano ya TAZARA ambapo jumla ya shilingi bilioni
moja (1) na milioni 26 zinatarajiwa kutumika katika kukamilisha mradi
huo.
Dkt. Mgimwa aliongeza kuwa eneo lingine ambalo litanufaika na msaada
kutoka Japan ni kuunga mkono sera ya Kilimo kwanza ambapo Tanzania
imepata shilingi bilioni sita(6) na milioni 92 kwa ajili ya kuhakikisha
kunakuwepo kwa usalama wa chakula cha kutosha katika maeneo mbalimbali
hapa nchini.
Alisema kuwa upande wa eneo hilo lengo ni kuhakikisha kuwa Watanzania
wengi wa kipato cha chini wanaboresha kilimo ambacho kitawahakikisha
uhakika wa chakula wakati wote na hivyo kuondokana na umaskini.
Kwa upande wa Balozi wa Japan hapa nchini Masaki Okada alisema kuwa
wananchi wengi wa Tanzania hasa wakazi wa Jiji la Dar es salaam wamekuwa
wakisubiri kwa hamu barabara za juu ili kusaidia kupunguza msongamano
wakati wa kuja na kutoka katikati ya jiji la Dar es salaam.
Alisema kuwa utakapo kamilika mradi huo utasaidia kupunguza tatizo la
msongamano na hivyo kupunguza saa za mwananchi kusafiri kuja na kutoka
katikati ya jiji la Dar es salaam.
Balozi Okada alisema kuwa hatua hii itakuwa muhimu katika kukuza uchumi
kwani wananchi watakuwa na muda wa kutosha kuzalisha mali kutoka na
miundombinu kuruhusu magari kwenda kasi pasipo kikwazo.
0 Comments