Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeridhia mapendekezo ya Kamati ya Mashindano ya kutaka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwa na timu 20 badala ya 18 za sasa.
Lengo la mabadiliko hayo ni Ligi ya Taifa (NL) kuchezwa kwa kanda, hivyo
msimu huu timu mbili zaidi (ukiondoa tatu ambazo zimeshapanda kutoka NL) zitaongezwa ili kufikisha idadi ya timu 20 katika FDL.
Timu ambazo zimepanda kutoka NL iliyochezwa katika vituo vitatu ni; Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoongoza Kituo cha Kigoma, Ndanda SC ya Mtwara iliyoibuka kinara Kituo cha Mtwara na Polisi Mara iliyokamata usukani katika Kituo cha Musoma.
Kamati ya Utendaji pia imepitisha mapendekezo ya kuchezwa play off ili kupata timu mbili zaidi za kucheza FDL msimu huu. Timu zitakazocheza play off katika utaratibu utakaotangazwa baadaye na Kamati ya Mashindano ni tatu zilizoshuka kutoka FDL na tatu nyingine zilizoshika nafasi za pili katika NL kutoka vituo vya Kigoma, Mtwara na Musoma.
Timu tatu zilizoshuka FDL ni AFC ya Arusha, Samaria ya Singida na Temeke United ya Dar es Salaam wakati zilizoshika nafasi za pili katika NL na vituo vyao kwenye mabano ni Kurugenzi ya Iringa (Mtwara), Mwadui ya Shinyanga (Kigoma) na Tessema ya Dar es Salaam (Musoma).
Hata hivyo, timu zitakazoshuka kutoka Ligi Kuu bado zitaendelea kuwa tatu kama ilivyo kwa zitakazopandwa.
AWAMU YA KWANZA USAJILI MWISHO AGOSTI 10
Kipindi cha kwanza cha usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2012/2013 kitamalizika Agosti 10 mwaka huu kulingana na kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya 2012/2013.
Uhamisho wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuacha wachezaji (sio wa Ligi Kuu. Wachezaji wa Ligi Kuu wanacheza kwa mikataba) ni kuanzia Juni 15- 30 mwaka huu.
Kwa klabu za Ligi Kuu kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka huu.
Tunasisitiza kipindi cha usajili kiheshimiwe na mikoa yote kwa sababu usajili huo huo ndiyo utakaotumika katika michuano ya Kombe la FA. Kwa maana nyingine hakutakuwa na kipindi kingine cha usajili wa wachezaji kwa klabu zote nchini hadi hapo litakapofunguliwa dirisha dogo.
Mechi ya kufungua msimu ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, timu ya Simba na makamu bingwa Azam itachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati Ligi Kuu itaanza Septemba Mosi mwaka huu, na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yenyewe itaanza Septemba 15 mwaka huu.
Ratiba ya Ligi Kuu itatolewa Julai 23 mwaka huu.
MISRI YAOMBA KUIKABILI NGORONGORO HEROES
Chama cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kimeomba mechi mbili za kirafiki kwa timu yao ya vijana na timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (Ngorongoro Heroes).
EFA imeomba mechi hizo zichezwe Julai 3 na Julai 5 mwaka huu kwa masharti maalumu. Ikiwa zitachezwa Misri, mwenyeji (EFA) atagharamia Ngorongoro Heroes kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya kufanyia mazoezi.
Ikiwa mechi hizo zitachezwa Dar es Salaam, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) litaigharamia timu ya Misri kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya mazoezi. Hivyo kila timu itajigharamia kwa usafiri wa ndege na posho kwa timu yake.
Sekretarieti ya TFF inafanya uchambuzi wa gharama ili kujua ipi ni nafuu kabla ya kufanya uamuzi wa wapi mechi hizo zichezwe.
Ngorongoro Heroes imeingia raundi ya pili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani nchini Algeria baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya kwanza.
Itacheza mechi ya kwanza ya raundi ya pili Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itakuwa Agosti 11 mwaka huu nchini Nigeria.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
0 Comments