KUONA TAMASHA LA PASAKA SH.2,000

Na Mwandishi Wetu
MASHABIKI watakaofika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia onesho la tamasha la Pasaka linalotarajiwa kufanyika Aprili 8 mwaka huu, watalazimika kulipa kiingilio kidogo cha sh. 2,000 na sh. 5,000 kwa viti vya kawaida.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama wa Kampuni ya Msama Promotions, alisema Dar es Salaam jana kuwa wametenga viingilio katika kategoria tatu tofauti.
 Msama alisema watoto watalipa sh. 2,000, mashabiki watakaokaa viti maalumu watalipa sh. 10,000 na watakaokaa viti vya kawaida watalipa sh. 5,000, na tiketi za kategoria zote hizo zitauzwa mlangoni.
Alisema tiketi za viti maalumu watakaohitaji wanaweza kupiga simu selula 0713 383838, 0786 383838 na 0786 373737 ili kupata tiketi na maelezo kinagaubaga.
"Tumeamua kuweka kiingilio kidogo cha wastani ili kila apate fursa ya kushuhudia tamasha la Pasaka wakiwamo watoto," alisema Msama.
 Msama alisisitiza kuwa tamasha hilo litahudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa kutoka ndani na nje ya nchi.
 Alisema tamasha hilo lina lengo la kuchangia watoto yatima ambao wazazi wao wamefariki kwa ugonjwa wa ukimwi na mitaji ya wanawake wajane wasiojiweza.
Fedha zilizopatikana katika tamasha la mwaka jana zilitumika kuwasaidia waathirika wa mabomu yaliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Gongo la Mboto, Dar es Salaam na pia kuwapa mitaji wajane wasiojiweza.
Baadhi ya wasanii wa nyimbo za Injili waliothibitisha kupamba tamasha hilo mwaka huu ni Upendo Kilahiro, Upendo Nkone, Atosha Kissava na kundi la Glorious Celebration.

Post a Comment

0 Comments