PRECISIONAIR YAISADIA TIKETI TWIGA STARS

Kampuni ya ndege ya PrecisionAir imetoa msaada wa tiketi zenye thamani ya sh. milioni 27.8 kwa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars) ambayo Januari 14 mwaka huu itacheza na Namibia jijini Windhoek kuwania nafasi ya kucheza fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC).
 
Akitangaza msaada huo leo (Januari 6 mwaka huu) kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Dar es Salaam, Meneja Mauzo wa PrecisionAir, Tuntufye Mwambusi amesema wameamua kusaidia kwa vile Twiga Stars imekuwa ikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali inayoshiriki.
 
Mwaka juzi Twiga Stars ilicheza fainali za AWC zilizofanyika Afrika Kusini, Julai mwaka jana ilikuwa kwenye michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) nchini Zimbabwe na kushika nafasi ya tatu wakati Septemba mwaka jana ilishiriki michezo ya Afrika (All African Games- AAG) jijini Maputo.
 
Mwambusi amesema tiketi hizo ni kwa ajili ya kuitoa Twiga Stars kutoka Dar es Salaam- Johannesburg- Dar es Salaam kwa ndege yao ya PrecisionAir. Awali PrecisionAir ilitoa punguzo la nauli kwa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) iliyoshiriki michuano ya COSAFA nchini Botswana.
 
Amesema mpango wa kampuni yake ni kushirikiana na TFF katika kuisafirisha Twiga Stars na timu za Taifa za vijana (Ngorongoro Heroes) na ile ya umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) kwenye nchi ambazo ndege yao inafika.
 
Naye Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah ameishukuru PrecisionAir kwa msaada huo mkubwa na pia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa kutoa kambi kwa Twiga Stars ambayo inatarajia kuondoka Januari 12 mwaka huu kwenda Namibia na kurejea Januari 15 mwaka huu.
 
Amesema TFF bado inahitaji msaada wa kuisafirisha timu hiyo kutoka Johannesburg hadi Windhoek na kurudi Johannesburg ambapo itachukuliwa na PrecisionAir. Jumla ya nauli pekee kwa Twiga Stars kutoka Dar es Salaam hadi Namibia na kurudi ni sh. milioni 36.
 
Hivyo amewataka wadau kusaidia nauli hiyo ya kutoka Johannesburg hadi Windhoek, gharama za malazi timu ikiwa Namibia na posho kwa wachezaji na benchi la ufundi ambapo jumla yao ni watu 25.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Post a Comment

0 Comments