KILA LA KHERI SIMBA NA YANGA

KIKOSI CHA TIMU YA YANGA KUKIPIGA LEO U/TAIFA DAR ES SALAAM
KIKOSI CHA TIMU YA SIMBA WATAKAOCHEZA COMORO
Na Dina Ismail
Wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa timu za Yanga na Simba leo zinashuka katika viwanja tofauti kutupa karata zao katika michuano hiyo.
Wakati Simba inayoshiriki ligi ya mabingwa barani Afrika itashuka nchini Comoro kukwaana na Elan de Mitsoudje ya huko, Yanga inayoshiriki kombe la Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), itakipiga na Dedebit ya Ethiopia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, makocha wa Yanga Fred Felix ‘Minziro’ na yule wa Dedebit, Gramme Haile, kila mmoja alijinasibu kutoka kifua mbele katika mechi ya leo.
Minziro, kocha msaidizi wa Yanga alisema, ana uhakika na kikosi chake kushinda mechi ya leo, kwani kwa kipindi kifupi alichokaa nacho ameona kina ubora wa kuweza kuwafunga wapinzani wao.
Alisema, ingawa wapinzani wao hao ni wazuri, lakini kwa kiasi kikubwa amekiandaa kikamilifu kikosi chake kukabiliana na mashambulizi ya aina yoyote toka kwa Wahabeshi hao.
“Tunafahamu wapinzani wetu ni wazuri lakini ninaimani na kikosi changu kwani kipo katika hali nzuri tayari kwa mechi ya kesho (leo), tunaomba dua za WAtanzania,” alisema Minziro.
Minziro aliongeza kuwa wachezaji wote wapo katika hali nzuri isipokuwa Ernest Boakye ambaye amechanika nyama za paja.
Katika kuhakikisha Yanga kesho inafanya kweli, mfadhili wa klabu hiyo, Yussuf Manji jana jioni aliwatembelea wachezaji kambini kuwaongezea morali ya ushindi.
Naye kocha wa Dedebit, Haile alisema kwamba ingawa hawafahamu vizuri Yanga, amekiandaa vema kikosi chake ambako ana imani wataibuka na ushindi mnono.
Kocha huyo aliongeza kuwa, wanataka kushinda mechi hiyo ya ugenini ili kujiwekea mazingira mazuri katika mechi ya marudiano itakayopigwa kwao baada ya wiki mbili.
Katika hatua nyingine, Meneja wa Simba Innocent Njovu alisema kikosi cha timu hiyo kipo katika hali nzuri tayari kwa mechi yao ya leo dhidi ya wenyeji wao, Elan.
Njovu alisema, kutokana na maandalizi yao pamoja na ari waliyonayo wachezaji, wana uhakika watashinda mechi hiyo ambayo pia inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na ubora walionao wapinzani wao.
“Timu yetu ipo katika hali nzuri na wachezaji wana ari ya kushinda kwa kishindo...ila kwa upande mwingine mechi yetu inatarajiwa kuwa ngumu kutokana na ubora walionao
wenzetu”, alisema Njovu.

Post a Comment

0 Comments