DKT. SAMIZI: SERIKALI YAIMARISHA MIKAKATI KUPUNGUZA UDUMAVU KWA WATOTO HADI ASILIMIA 20 IFIKAPO 2030.

 


Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na udumavu kwa watoto chini ya miaka mitano, ikilenga kupunguza kiwango cha udumavu kutoka asilimia 30 ya sasa hadi asilimia 20 ifikapo mwaka 2030.


Mikakati hiyo imeelezwa leo, Novemba 3, 2026, bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Dkt. Catherine Canute Joachim, aliyetaka kujua mkakati wa Serikali wa kupunguza kiwango cha udumavu nchini.


Dkt. Samizi amesema katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali inatekeleza Mpango Jumuishi wa Pili wa Taifa wa Lishe wa mwaka 2021/22 hadi 2025/26, unaojumuisha uhamasishaji wa ulishaji sahihi wa watoto, ikiwemo unyonyeshaji na kuanza kuwapa vyakula vya nyongeza wanapofikisha umri wa miezi sita, huku wakiendelea kunyonya hadi miaka miwili au zaidi.


Amesema Serikali pia inaendelea kutoa elimu ya lishe katika vituo vya kutolea huduma za afya na kuhamasisha jamii kupitia vyombo vya habari, ikiwemo redio, televisheni na mitandao ya kijamii, pamoja na kutoa elimu kwa wajawazito, wazazi na walezi wanapohudhuria kliniki.


Aidha, amesema mikakati mingine inayotekelezwa ni utoaji wa matone ya Vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto chini ya miaka mitano, uongezaji wa virutubishi vya madini na vitamini katika vyakula kama mafuta ya kula, unga wa ngano, unga wa mahindi na chumvi, pamoja na utoaji wa vidonge vya madini chuma na asidi ya foliki kwa wanawake wajawazito.


Ameeleza kuwa Serikali imedhamiria kuhakikisha ifikapo mwaka 2050, utapiamlo wa aina zote unatoweka au unapungua hadi kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa kuwa havina madhara kwa jamii.

Post a Comment

0 Comments