DC KAHAMA ATATUA MGOGORO WA ENEO LA GULIO KAGONGWA



Kahama  

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Dkt. Francis Daudi, amefika katika Kata ya Kagongwa kutatua mgogoro wa matumizi ya eneo la gulio lililopo Mtaa wa Kagongwa, kufuatia changamoto zilizojitokeza kuhusu eneo hilo kati ya wananchi na wafanyabiashara wadogo.

Katika hatua ya kutafuta suluhu ya kudumu, Dkt. Daudi amekutana na wananchi pamoja na wafanyabiashara wadogo na kufikia makubaliano ya kuhamishia gulio hilo katika eneo jingine lenye nafasi ya kutosha ili kuwezesha shughuli za biashara kufanyika katika mazingira bora na yenye utaratibu.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ameelekeza miundombinu yote muhimu inayohitajika katika eneo jipya la gulio kukamilishwa ndani ya kipindi cha wiki mbili, ili kuruhusu shughuli za gulio kuanza mara moja baada ya maandalizi hayo kukamilika.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wanapata eneo rafiki la kufanyia biashara, huku wananchi wakipata huduma katika mazingira yanayozingatia mahitaji ya jamii na utaratibu wa matumizi ya maeneo ya umma.


Akisisitiza umuhimu wa kutatua changamoto za wananchi kwa njia ya mazungumzo na makubaliano, Dkt. Daudi ameendelea kuhimiza ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika kuimarisha mazingira ya biashara na kuchochea maendeleo ya Wilaya ya Kahama na kauli mbiu isemayo Kahama ni Ardhi ya Fursa.

Post a Comment

0 Comments