Na Emmanuel Buhohela - Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amesema ongezeko la idadi ya Wanyamapori katika hifadhi za Wanyama hapa nchini imetokana na juhudi za serikali kushirikisha wadau wa uhifadhi wa Wanyamapori na wananchi kwa ujumla hali iliyopelekea kukua kwa utalii na uchumi katika Taifa.
Ameyasema hayo leo Machi 03, 2025 jijini Dodoma katika maadhimisho ya 11 ya Siku ya Wanyamapori Duniani ambapo amesisitiza Tanzania inaongoza Duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama aina ya Simba, Chui, Nyati na ni ya tatu kwa idadi wa Tembo Duniani huku akifafanua kuwa mafanikio hayo ni kutokana na kuitangaza vyema sera ya Utalii ndani na nje ya nchi na kuboresha jeshi la uhifadhi.
“Wanyamapori ni rasilimali muhimu katika uchumi wa nchi yetu kupitia utalii ambao unachangia zaidi ya asilimia 25 ya fedha za kigeni, asilimia 17.1 ya Pato la Taifa na ajira takribani milioni 1.6 zilizo rasmi na zisizo rasmi, hadi Mwaka 2024, Sekta ya Utalii imevunja rekodi kwa kufikia jumla ya watalii 5,360,247 na watalii wa Kimataifa imefikia 2,141,895 huku watalii wa ndani wakiwa 3,218,352. Kutokana na mapato ya utalii imefikia Dola za Marekani Bilioni 3.9” Amesema Waziri Chana
Aidha, ameweka bayana kuwa juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kwa vitendo ndani na nje ya nchi kupitia Programu ya Tanzania the Royal Tour na Amazing Tanzania imesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa kwa watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea hifadhi za utalii na Wanyamapori hapa nchini.
Katika hatua nyingine, Waziri Dkt. Chana amesema Serikali kupitia Wizara Hiyo imeendelea kushirikiana na wadau wa uhifadhi kuchukua jitihada za makusudi ikiwemo kulinda na kuendeleza uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori, kudhibiti ujangili wa nyara na kitoweo na uhifadhi endelevu wa mapito ya wanyamapori ili kuimarisha mifumo ikolojia ya uhifadhi sambamba na ushirikishwaji wa jamii kupitia maeneo ya Jumiya za Hifadhi za Wanyamapori.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Alexander Lobora amesema lengo la siku hiyo ni kuhamasisha Jamii juu ya Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na mimea iliyohatarini kutoweka, kupunguza uharibifu wa mazingira na kupinga ujangili.
.jpg)



0 Comments