TMDA YATOA UFAFANUZI UVUMI WA DAWA YA PARACETAMOL INAYODAIWA KUBABUA NGOZI


Na Andrew Chale 

MAMLAKA ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA)iliyo chini ya Wizara ya Afya, imetoa taarifa kwa Umma ufafanuzi kuhusu uvumi juu ya Dawa ya Paracetamol inayodaiwa kubabua ngozi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kwa Umma liyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo Imebainisha kuwa, imebaini uwepo wa taarifa inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwepo wa dawa aina ya Paracetamol ambayo imeandikwa P 500 na 
kudaiwa kubabua ngozi kama inavyooneshwa (pichani).

Akinukuu taarifa hiyo inayosambazwa mitandaoni:

"Dawa hiyo 
inadaiwa kuwa ni ‘’paracetamol mpya nyeupe sana na inayong'aa, madaktari 
wanashauri kuwa ina virusi vya "Machupo", inayochukuliwa kuwa moja ya virusi 
hatari zaidi ulimwenguni, na kiwango cha juu cha vifo.

Aidha, Mtoa taarifa anaitaka jamii kuisambaza taarifa hii kwa kila mtu aliyeko katika orodha 
yake ya mawasiliano ili kuokoa maisha. Anamalizia kwa kusema ‘’Nimefanya 
sehemu yangu, sasa ni zamu yako. Kumbuka kwamba Mungu huwasaidia wale 
wanaosaidia wengine. ‘’Sambaza kama ilivyopokelewa’’.

Dkt.Fimbo ameeleza kuwa, Taarifa hiyo imekuwa ikijirudia mara kwa mara na TMDA imekuwa ikitolea ufafanuzi
ikiwemo taarifa ya mnamo tarehe 10 Mei, 2023, juu ya dawa aina ya P-500® 
(PARACETAMOL) ya Apex Laboratories Private Limited, Tamil Nadu, India 
iliyodaiwa kuwa na virusi hivyo.

"TMDA inapenda kuufahamisha Umma kwa mara nyingine kwamba hakuna virusi 
vinavyojulikana kwa jina la Machupo. Aidha, virusi vya aina yoyote haviwezi kuishi kwenye kidonge. 

Dawa zenye kiambata hai cha paracetamol inayotumika kutibu homa na maumivu 
zilizopo katika soko nchini kwa majina mbalimbali ya kibiashara zimesajiliwa baada 
ya kuthibitishwa kuwa zinakidhi vigezo vya usalama, ubora na ufanisi unaotakiwa na 
hivyo, ni salama kwa matumizi yaliyoainishwa. 

Katika hatua hiyo, TMDA inapenda kuwahakishia wananchi kuwa inaendelea kutimiza wajibu wake wa 
kulinda afya ya Jamii kwa kuhakikisha kuwa bidhaa tiba zinazotumika nchini ni zile 
zenye kukidhi matakwa ya ubora, usalama na ufanisi.

Vilevile, Mamlaka inapenda kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kupata ufafanuzi 
kutoka kwenye mamlaka husika kabla ya kusambaza taarifa zinazoweza kuleta 
taharuki kwenye Jamii.

TMDA
yenye jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa tiba nchini ambapo Ili kuhakikisha kuwa bidhaa tiba (zikiwemo dawa) zilizoko katika soko nchini zinakidhi matakwa ya usalama, ubora na ufanisi, TMDA imeweka mifumo mbalimbali 
ya udhibiti ikiwa ni pamoja na tathmini na usajili, ukaguzi, uchunguzi wa kimaabara 
na ufuatiliaji wa ubora na usalama wa bidhaa katika soko. 

Aidha, Wananchi wanaweza kupiga simu ya bila malipo: 0800110084 endapo wapatapo taarifa za mashaka kama hizo.


Post a Comment

0 Comments