MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI SIMBA

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu rambirambi kwa Rais wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Evans Aveva kutokana kifo cha shabiki wa timu hiyo, Shose Fideline aliyefariki dunia jana mchana Mei 28, 2017 katika ajali ya gari.

Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu za pole kwa majeruhi katika ajali hiyo akiwamo Nahodha wa Simba, Jonas Mkude na dereva wa gari hilo ambalo lilikuwa safarini kurejea Dar es Salaam kutoka Dodoma. Wanafamilia kadhaa wa mpira wa miguu walikuwa Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita kushuhudia mchezo wa fainali za Kombe la Azam - ASFC (Azam Sports Federation Cup HD 2016/17) uliozikutanisha timu za Simba na Mbao FC ya Mwanza.

Mbao ilifungwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa dakika 120. Gari lililopata ajali ni aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilianguka na kuzunguka mara kadhaa na baadaye kutulia katika eneo la Dumila mkoani Morogoro baada ya tairi yake ya nyuma kupasuka hivyo kumshinda dereva na kupoteza mwelekeo kutoka barabara kuu.
“Nakuandikia Rais wa Simba, Evans Aveva, pia ndugu, jamaa na marafiki pamoja na majirani wa marehemu Shose Fideline na wanafamilia wengine wa mpira wa miguu, kwamba nimepokea taarifa za ajali ya gari iliyosababisha kifo cha mmoja wa mashabiki wa timu ya Simba kwa masikitiko makubwa sana.

Wito wangu, nawaomba wanafamilia wote kuwa watulivu na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Rais Malinzi.

Msiba wa shabiki huyo wa Simba umetokea wakati Simba imetawazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la Azam likihitimisha ushindani wa timu 86 na hivyo kuwa na hati ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) hapo mwakani. Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema, Shabiki wa Simba, Shose Fideline.

“Pia nawapa pole nyingi sana majeruhi wote katika ajali hiyo akiwamo Jonas Mkude ambaye ni Nahodha wa Simba na Nahodha Msaidizi wa Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wapone haraka ili kujiunga na shughuli zao mbalimbali za ujenzi wa nchi,” amesema Rais Malinzi.

Kadhalika, Rais Malinzi ameipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa huo wa ASFC hivyo pamoja na zawadi nyingine kama vile Sh 50 milioni na medali za ubingwa pia Simba imepata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Shirikisho - michuano inayoandaliwa na CAF.
“Naitakia Simba maandalizi mema ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani,” amesema Rais Malinzi.

TAIFA STARS KUWEKA KAMBI MISRI, MKUDE ABAKI

 Kikosi cha wachezaji 20 wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kinachodhaminiwa na Kampuni ya Bia ya Serengeti, kinatarajiwa kuondoka kesho Jumanne saa 10.45 jioni kwenda Misri.

Taifa Stars ambayo itakuwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa kesho saa 7. 45 mchana inakwenda Misri kufanya kambi ya siku nane kujindaa na mchezo dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Wachezaji hao 20 kutoka hapa Tanzania wataungana na na wengine watatu, Nahodha Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Faridi Mussa wanaocheza ughaibuni katika kikosi hicho na kufanya jumla ya wachezaji kuwa 23 nchini Misri.
Nahodha Msaidizi, Jonas Mkude hatakuwako kwenye msafara huo kutokana na ushauri wa madaktari walioelekeza kwamba nyota huyo wa Simba apate mapumziko ya angalau siku nne.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga ameridhia na kusema kuwa Mkude ataungana na wenzake Juni 8, mwaka huu timu itakaporejea kutoka Misri.
Mayanga hajajaza nafasi ya Mkude.

 Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika nchini Cameroon. Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo. Kikosi cha Taifa Stars kinachofundishwa na Kocha Salum Mayanga kinaundwa na makipa Aishi Manula (Azam FC), Benno Kakolanya (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar). Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Kapombe (Azam FC) na Hassan Kessy (Yanga SC) wakati upande wa kushoto wapo Mohammed Hussein (Simba) na Haji Mwinyi (Yanga SC).

Walinzi wa kati Erasto Nyoni (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Agrey Morris (Azam FC) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye hatasafiri na timu kwa sasa.
Viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania). Washambuliaji wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting). Wasaidizi wa Mayanga katika benchi la ufundi ni Novatus Fulgence ambaye ni kocha msaidizi Patrick Mwangata - kocha wa makipa pia yumo Meneja wa timu, Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu, Daktari wa timu ni Richard Yomba na Daktari wa viungo ni Gilbert Kigadya. Timu hiyo iliingia kambini Machi 23, 2017 kwenye Hoteli ya Urban Rose, Dar es Salaam kabla ya kesho kwenda Misri na baadaye itarejea Tanzania kucheza na Lesotho, Juni 10, mwaka.


MAREKEBISHO YA KANUNI ZA LIGI KUU YA VODACOM NA LIGI DARAJA LA KWANZA

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linatangazia klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2017/18 na zile za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2017/18 kwamba kipindi hiki ni cha kuwasilisha maoni na mapendekezo mbalimbali kuhusu marekebisho ya kanuni za ligi husika.

TFF inaagiza klabu zote - kwa nafasi walizonazo kama wanafamilia ya mpira wa miguu, kuwasilisha mapendekezo na maoni kuhusu marekebisho ya katiba kwa njia ya kuyatuma kupitia anwani za sanduku la Barua 1574, Dar es Salaam au barua pepe tplb.tplb@yahoo.com au yaletwe moja kwa moja ofisi za Bodi ya Ligi au TFF. Maoni hayo tayafanyiwa kazi na Bodi ya Ligi kabla ya kupelekwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji kabla ya kuanza msimu husika wa mashindano baada ya kupita msimu uliopita.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

Post a Comment

0 Comments