Umoja wa Viongozi wa madhehebu ya dini nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati wameonesha imani kubwa ya ulinzi wa amani unaotolewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania nchini humu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kutembelewa na Kamanda wa Kikosi cha Nane cha Ulinzi wa Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Luteni Kanali Theofili Nguruwe wamesema uwepo wa JWTZ umekuwa na tija sana nchini humo kwani wamekuwa wakifanya kazi zao kwa weledi wa hali ya juu.
Sheikh Rashid Mohamoud Arouna ni Imam wa Masjid Nuur amesema JWTZ limekuwa mstari wa mbele kwenye kila jambo ambalo wanaombwa kutoa msaada kwa ajili ya kuhakikisha nchi yao inakuwa na amani.
Akizungumza kwa niaba ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Berberati Mhashamu Koffi Denis, Karibu Mkuu wa Jimbo hilo Padre Jean Ancelimo amesema mbali na Ulinzi wa Amani pia limekuwa likitoa misaada mbalimbali ya hali na mali huku akitolea mfano wa ujenzi wa shule ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambayo imepewa jina la Serengeti.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Evenjeliko (AEC) Mhashamu Lucian Nday amesema uwepo wa JWTZ nchini hapo umewafanya waishi kwa amani na zaidi ya yote limewezesha ukuaji wa lugha adhimu ya kiswahili.
Kwa upande wa Kamanda wa Kikosi cha Nane cha Ulinzi wa Amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati Luteni Kanali Theofili Nguruwe amewashukuru viongozi hao na kuahidi kutekeleza majukumu yake kwa weledi wa hali ya juu.
0 Comments