Watuhumiwa wa kesi ya kujihusisha na rushwa ya Shilingi Milioni 50 kutoka Kampuni ya Glenn Glarke, Edward Magobela (mbele) ambaye ni mfanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart akiwa na mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Mkwizu wakiingia katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
(Picha na Francis Dande)
+255784 62 39 58
+255713 62 39 58
www.francisdande.blogspot.com
Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewapandisha kizimbani kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu maofisa wawili akiwemo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Aman Mkwizu kwa kujihusisha na rushwa ya Sh.milioni 50.
Mbali ya Mkwizu, ofisa mwingine ni mfanyakazi wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart&Co.Ltd, Edward Mwagobela ambao walisomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Denis Lekayo.
Akiwasomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Huluma Shahidi, Wakili Lekayo alidai washtakiwa walijihusisha na vitendo hivyo kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa mnamo Aprili 19, mwaka huu katika jiji la Dar es Salaam maofisa hao walijihusisha na vitendo vya rushwa ya Sh.milioni 50 ili kupunguza gharama ya kodi ya Sh.milioni 375 hadi kufikia Sh.milioni 100.
Inadaiwa walichukua kiasi hicho kutoka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Commercial Salles &Service Ltd, Glenn Clarke. Katika kosa la pili, inadaiwa Aprili 19, mwaka huu kwa pamoja walijihusisha na rushwa ya Sh.milioni tano ili kupunguza gharama hiyo ya kodi kinyume na taratibu za waajili wao.
Shtaka la tatu inadaiwa ndani ya Aprili 19, mwaka huu walijihusisha tena na rushwa ya Sh.milioni 3 ikiwa malipo ya kupunguza gharama ya kodi ya Sh.milioni 375 hadi kufikia Sh.milioni 100.
Baada ya kusomewa maelezo hayo, washtakiwa walikana mashtaka, ambapo Wakili wa Serikali alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hata hivyo, washtakiwa hao walirudishwa lumande hadi Mei 9, mwaka huu baada ya kushindwa kutimizia masharti ya dhamana ya wadhamini wawili watakaosaini Sh.milioni 100.
Wakati huo huo, Upande wa Jamhuri katika kesi ya kusafirisha nje ya nchi meno ya tembo yenye thamani ya Sh5.4 bilioni inayowakabili watu watatu, akiwamo raia wa China, Yang Glan umesema upelelezi umekamilika.
Watuhumiwa wengine wanaokabiliwa na kesi hiyo ni wafanyabiashara Salivius Matembo na Philimon Manase, ambao wanadaiwa kujihusisha na biashara ya nyara za serikali, uhujumu uchumi na kutoroka chini ya ulinzi halali wa askari.
Wakili wa Serikali, Salim Msemo aliieleza mahakama mbele ya Hakimu Mkazi Huluma Shahidi kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika, hivyo wanasubiri kupangiwa tarehe ya kumsomea mshtakiwa mashtaka.
Hakimu Shahidi alisema kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo itasubiri kibali cha Mkurugenzi wa Mashtka (DPP) kama itawaruhusu waisikilize kesi hiyo au lah. Alisema kutokana na sababu hizo, kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 9, mwaka huu ili kuanza kuisoma endapo kibali kikitoka.
Hata hivyo, mshtakiwa Glan aliilalamikia mahakama kwa kuahirisha kesi yake mara kwa mara na kucheleweshwa usikilizaji. Pia alidai afya yake sio nzuri kwani anasumbuliwa na ugonjwa moyo na amekaa muda mrefu gerezani.
“Naiomba Mahakama inisaidie ikiwezekana nipelekwe pale Hospitali ya Taifa Muhimbili maana kuna kitengo cha kutibu magonjwa ya moyo, kwani tangu nipimwe kule gerezani Daktari ananambia aataniangalia lakini haikuwa hivyo,” alieleza.
Watu hao wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari Mosi, 2000 na Mei 22, 2014 jijini Dar es Salaam, walijihusisha kuendesha biashara ya vipande 706 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh5,435,865,000.
0 Comments