Naibu wa Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi (kulia) akitoa mada katika Mkutano wa Afya kati ya nchi za Afrika na Nodiki jijini Stockholm, Sweden.
Stockholm, Sweden.
Ubalozi wa Tanzania nchini Sweden umer
atibu ushiriki wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uzinduzi wa Mkutano wa Afya kati ya nchi za Nodiki na Afrika uliofanyika tarehe 22 Januari, 2026, jijini Stockholm, Sweden, ili kujadiliana masuala ya afya ya uzazi na mtoto na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo uliongozwa na Naibu wa Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi akiambatana na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).
Wataalamu hao ni Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Uzazi na Mama, Dkt. Mzee Nassoro; Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza na Afya ya Akili, Dkt. Omary Ubuguyu; Mkurugenzi wa Huduma za Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya ya SMZ, Dkt. Salim Slim; na Mhadhiri Mwandamizi wa MUHAS, Dkt. Amani Idris Kikula.
Mkutano huo uliandaliwa kwa ushirikiano kati ya kundi la Mabalozi Wanawake wa nchi za Afrika waliopo kwenye nchi za Nodiki na taasisi za afya za Nodiki na kimataifa za Maternity Foundation, Dalberg Media, Danish Alliance for Global Health, Global Financing Facility, World Diabetes Foundation, Ferring Pharmaceuticals na Laerdal Global Health.
Viongozi mbalimbali wa serikali za nchi za Nodiki walishiriki na kuzungumza wakiwemo Waziri wa Afya na Masuala ya Kijamii wa Sweden, Mhe. Jakob Forssmed; Waziri wa Usawa wa Kijinsia wa Sweden, Mhe. Nina Larsson; Naibu Waziri wa Afya na Masuala ya Kijamii wa Sweden, Mhe. Petra Noreback; Naibu Waziri wa Sera za Maendeleo wa Denmark, Mhe. Elsebeth Sondergaard Krone na maafisa waandamizi wa serikali za Norway na Finland pamoja na mashirika ya kimataifa.
Aidha, Waziri wa Afya wa Zimbabwe, Mhe. Dkt. Douglas Mombeshora, naye alihudhuria pamoja na viongozi wengine wa sekta ya afya kutoka Nigeria, Liberia, Rwanda na Kenya na vilevile Afisa Mtendaji Mkuu wa Amref Health Africa, Bw. Githinji Gitahi na Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, Dkt. Ntuli Kapologwe (ECSA-HC).
Katika tukio jingine siku hiyo hiyo lililoandaliwa na Mradi wa Goalkeepers unaodhaminiwa na Mfuko wa Gates kupambania Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG), Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark, Mhe. Lars Lokke Rasmussen na Bill Gates nao pia walihudhuria na kuzungumza.
Wakati akiwasilisha mada katika mkutano huo, Mhe. Naibu Waziri Dkt. Samizi alielezea mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya afya chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya na ununuzi wa vifaa vya tiba vya kisasa katika ngazi zote za hospitali nchini.
Dkt. Samizi alielezea kuwa kati ya mwaka 2015 hadi 2022 Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kutoka vifo 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000, ambapo katika kipindi hicho pia vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000, huku vifo vya watoto wachanga vikishuka kutoka 25 hadi 24 kwa kila vizazi hai 1,000.
Aidha, Dkt. Samizi alitumia fursa hiyo kuzikaribisha nchi za Nodiki kuwekeza nchini katika sekta ya afya na kushirikiana katika tafiti, teknolojia na uzalishaji wa dawa na vifaa vya tiba. Nchi za Sweden na Denmark zilieleza kuwa zipo tayari kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo Tanzania kulingana na vipaumbele vya kisera.
Imetolewa na:
Ubalozi wa Tanzania wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden
23 Januari 2026.
Naibu wa Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi (kulia) akijadiliana jambo na Mkunga Mkuu wa Shirikisho la Wakunga la Kimataifa (ICM), Prof. Jacqueline Dunkley-Bent, wakati wa Mkutano wa Afya kati ya nchi za Afrika na Nodiki jijini Stockholm, Sweden. Katikati ni Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi.
Naibu wa Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi (wa pili kushoto) akiwa na Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi (wa pili kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Kinga na Elimu ya Afya wa Wizara ya Afya ya SMZ, Dkt. Salim Slim (kushoto), na Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Afya ya nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, Dkt. Ntuli Kapologwe (kulia), wakati wa Mkutano wa Afya kati ya nchi za Afrika na Nodiki jijini Stockholm, Sweden.



0 Comments